Featured Kitaifa

WATAALAMU WA AFYA NCHINI WATAKIWA KUTUMIA MATOKEO YA TAFITI

Written by mzalendoeditor

Wito umetolewa kwa wataalamu wa afya nchini kuhakikisha wanatumia matokeo ya tafiti wanazofanya kuboresha mifumo ya afya nchini.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wakati akifungua Kongamano la kujadili matokeo ya utafiti wa ugonjwa wa Uviko 19 uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

“Napenda niwahimize watafiti wote kuhakikisha tafiti zao zinawafikia watumiaji, aidha nawasihi wataalamu wetu wahakikishe wanayatumia matokeo ya tafiti hizi ili kuboresha mifumo yetu ya afya nchini,” amesema Dkt. Mwinyi.

Rais Mwinyi ameipongeza familia ya hayati mama Amne Salim kupitia Mfuko wa Amne Salim kwa kufadhili tafiti hizo kwani kupitia matokeo ya tafiti hizo Serikali itapata kulielewa tatizo la ugonjwa huo na kufahamu njia ya kukabiliana nao kwa maslahi ya taifa.

“Taifa bora hujengwa na raia wenye afya. Hili litafikiwa iwapo tutafanya tafiti zinazoweza kutatua changamoto zinazotukabili na kutoa ushauri wa kitaalamu kupitia tafiti hizi” amesema Rais Mwinyi.

Kwa upande wake, Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuungana na Serikali kuwezesha tafiti mbalimbali kufanyika hasa za sayansi, uhandisi na elimu tiba.

Ameongeza kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya watafiti wanaofanya kazi katika Vyuo Vikuu nchini ambao wataweza kuchapisha tafiti zao kwenye majarida makubwa duniani, kila atakayechapisha tafiti katika majarida hayo atapata Shilingi milioni 50.

“Tunafanya hivyo ili watafiti waweke nguvu zao kwenye tafiti huku wakiendesha familia zao bila vikwazo, na katika bajeti ijayo tutatenga fedha zaidi kuendelea kuwezesha hilo,” amesema Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa Serikali imeanzisha ufadhili unaofahamika kama ‘Samia Scholarship’ ambao unawezesha wanafunzi waliofaulu vizuri katika masomo ya sayansi kuweze kuendelea na masomo ya chuo kikuu katika fani za uhandisi, sayansi na elimu tiba.

Naye Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Andrea Pembe amesema Mfuko wa Amne Salim wa Ufadhili wa Utafiti wa Uviko 19 ndio uliofadhili utafiti huo kwa lengo la kusaidia tafiti za kitabibu na kisayansi juu ya Uviko 19.

“Mfuko huu ulianza na Shilingi milioni 100 na baadae kampuni ya Karimjee Jivanjee ikaongeza dola 5,000. Fedha hizo ziligawiwa kwa watafiti wanane waliopatikana kupitia ushindanishi wa uwazi,” ameongeza Prof. Pembe.

Akiongea katika kongamano hilo, Ahmed Salim ambaye ni mwakilishi wa familia ya hayati Amne Salim amesema kama familia waliona kuna umuhimu wa kuufahamu zaidi ugonjwa wa Uviko 19 na athari zake hivyo wakaanzisha mfuko huo ili kuwezesha utafiti kufanyika juu ya ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa wanaamini kupitia matokeo hayo ya tafiti itasaidia watunga sera kutunga sera zenye tija, kulinda wanaoishi kwenye mazingira magumu na kuwezesha Serikali kuwa na utayari wa haraka kukabiliana na magonjwa kama hayo pindi yanapozuka.

About the author

mzalendoeditor