Featured Kitaifa

GGML,HALMASHAURI ZA GEITA ZASAINI MAKUBALIANO YA CSR YA THAMANI YA SH BILIONI 19

Written by mzalendoeditor
Mwanasheria Mkuu wa GGML, David Nzaligo (kulia) akisaini makubaliano hayo kwa niaba ya kampuni hiyo huku upande wa Halmashauri ya Mji Geita ukisainiwa na Mwanasheria wake na chini ya  Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Zahara Michuzi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Geita Gold Mining Limited, Elder Damon pamoja (kulia) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi (kushoto) wakionesha makubaliano waliyosaini kwa ajili ya utekeleza wa mpango huduma kwa jamii (CSR). GGML imetoa jumla ya Sh bilioni 19 kutekeleza makubaliano hayo ya CSR kwa mwaka 2022/2023. Anayeshuhudi katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela na maofisa wengine wa GGML na mkoa huo.
Mwanasheria Mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), David Nzaligo (kulia) akisaini makubaliano ya utekelezaji wa mpango wa huduma kwa jamii (CSR) kwa niaba ya kampuni hiyo leo Jumanne mjini Geita ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Geita imepata Sh bilioni 8.6 kati ya Sh bilioni 19 zilizotolewa kwa wilaya za mkoa huo. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Maghembe akimshuhudia mwanasheria wa wilaya hiyo akitia saini makubaliano hayo.
Mwanasheria Mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), David Nzaligo (kulia) akisaini makubaliano ya utekelezaji wa mpango wa huduma kwa jamii (CSR) kwa niaba ya kampuni hiyo leo Jumanne mjini Geita ambapo Wilaya ya Mbogwe imepata Sh 200 kati ya Sh bilioni 19 zilizotolewa kwa wilaya za mkoa huo. Kulia ni wawakilishi wa wilaya hiyo wakisaini makubaliano hayo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Geita Gold Mining Limited, Elder Damon pamoja (kulia) na wawakilishi wa wilaya ya Bukombe wakionesha mikataba ya makubaliano waliyosaini leo Jumanne mjini Geita kutekelezaji wa mpango wa huduma kwa jamii (CSR) wa GGML. Bukombe pia imepata Sh 200 kati ya Sh bilioni 19 zilizotolewa kwa wilaya za mkoa huo.
Mwanasheria Mkuu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), David Nzaligo (kulia) akisaini makubaliano ya utekelezaji wa mpango wa huduma kwa jamii (CSR) kwa niaba ya kampuni hiyo leo Jumanne mjini Geita ambapo Wilaya ya Chato imepata Sh 200 kati ya Sh bilioni 19 zilizotolewa kwa wilaya za mkoa huo. Kulia ni wawakilishi wa wilaya hiyo wakisaini makubaliano hayo.
NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na wenyeji wake Halmashauri ya Mji Geita, Wilaya ya Geita pamoja na Halmashauri za jirani za wilaya za Chato, Bukombe na Mbogwe kutekeleza Mpango wa Uwajibikaji wake kwa Jamii (CSR) kwa mwaka 2022/2023 wenye thamani ya Sh bilioni 19.
Jumla ya Sh bilioni 9.8 zimetengwa kwa ajili ya Halmashauri ya Mji wa Geita ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, bajeti ya Sh bilioni 8.6 imetengwa.
Katika makubaliano hayo GGML pia itatoa jumla ya Sh milioni 600 kutekeleza miradi ya maendeleo kwa halmashauri tatu za Mbogwe, Chato na Bukombe mkoani Geita ambapo kila moja itapata shilingi milioni 200. 
Makubaliano hayo yametiwa saini jana Machi 21, 2023 mjini Geita na kushuhudiwa na Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela, wakuu wa wilaya za mkoa huo na wadau wengine.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Geita Gold Mining Limited, Elder Damon alisema kutiwa saini kwa makubaliano hayo ni jambo muhimu na linathibitisha dhamira njema ya kampuni hiyo kwa jamii iliyowakaribisha, Serikali ya Tanzania na watu wake kwa kufuata matakwa ya Sheria ya Madini ambayo yanazingatia Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii.
 Alisema mpango wa CSR wa mwaka huu ni mwendelezo wa mipango ya awali unaolenga kujumuisha maendeleo yaliyofikiwa na GGML hadi sasa katika maeneo ya mazingira, miundombinu, afya, elimu na biashara ndogondogo na za kati (SMEs) katika jamii ya mwenyeji wa Geita. 
“Binafsi inanipa furaha kubwa kushuhudia matokeo ya miradi yenye mafanikio katika maisha ya Watanzania, hasa wale wanaoishi karibu na mgodi. GGML inajitahidi kuunga mkono matarajio ya Serikali ya Tanzania ya maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika jamii zinazowapokea. 
“Hii inaendana na thamani yetu ya msingi ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuzipatia jamii, tunamofanyia kazi, maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ambayo shughuli za uchimbaji madini zinafanyika.
Kwa hiyo, ninajivunia kwamba kutiwa saini kwa Makubaliano haya kunatokana na mchakato unaojumuisha pande zote kati ya Serikali, jamii mwenyeji na GGML. Ninaamini kuwa mchakato endelevu wa kufanya kazi pamoja utaimarisha umiliki wa mpango huu wa CSR na ule wa siku zijazo na hivyo utahakikisha mafanikio na uendelevu kwao,” alisema.
Aidha, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo alisema watu wengi hawafahamu kwamba kabla ya sheria ya madini ya mwaka 2010 kufanyiwa marekebisjo mwaka 2017, tayari GGML ilikuwa inatekeleza mpango wa CSR kwa kutoa zaidi ya Sh bilioni 9 kugharamia miradi mbalimbali ya kijamii mkoani Geita.
“Hata baada ya kuingiza kipengele hicho cha uwajibikaji wa kampuni kwa jamii -CSR, sisi tulikuwa wa kwanza kufanya hivyo kwani kila mwaka tunatumia walau Sh bilioni 9.2 hadi 10,” alisema Simon Shayo.
“Kipindi cha mwaka 2015 hadi 2017 tuliona ni muhimu kuongeza kwa kiasi kikubwa fedha tunazowekeza kwenye jamii ili kutengeneza uchumi mbadala hata mgodi ukifungwa,” alisema Shayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela, alisema ni furaha kushuhudia tukio hilo likifanyika kipindi ambacho wanaadhimisha miaka miwili tangu Serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Dkt. Samia Suluh Hassan kuanza kazi ya kuongoza taifa maendeleo yake ikiwemo ya sekta ya madini. 
“Nichukue pia fursa hii kuipongeza sana kampuni ya GGML kwa kuwa kinara wa uchimbaji endelevu wa madini. Nawashukuru pia kwa kuwa na subira na uungwana wa kutuvumilia kukamilisha mchakato wa utiliaji saini hii ya makubaliano ambao umekuwa ukisogezwa mbele mara kwa mara.Majadiliano na mapendekezo ambayo tumekuwa tukiyafanya baina ya pande zote mbili yaani sisi serikali na Uongozi wa GGML yameonyesha ukomavu mkubwa na wenye afya katika aina ya uwekezaji tunaoutaka katika taifa letu,” alisema.
Aidha, alitoa wito kwa wana-Geita kuchangamkia fursa za miradi hiyo kwa kuhakikisha mahitaji ya wakandarasi yanapatikana ndani ya mkoa huo.
Pia aliagiza viongozi wa halmashauri kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi ili kutoacha mapungufu yoyote.

About the author

mzalendoeditor