Featured Michezo

NAIBU WAZIRI MWINJUMA AFANYA ZIARA TaSUBa, AZUNGUMZIA MFUKO WA SANAA, UTAMADUNI

Written by mzalendoeditor


Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Hamis Mwinjuma maarufu kwa jina la Mwana FA amefanya ziara ya kutembelea Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) huku akitumia nafasi hiyo kueleza mipango inayoendelea katika kuongeza hadhi ya taasisi hiyo na wanaopata mafunzo waone fahari.

Aidha ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kutoa fedha za moja kwa moja kwa watu wanaojishughulisha na shughuli za Sanaa na utamaduni kupitia mikopo inayotolewa kwa kutumia Mfuko wa Utamaduni na Saaa ambapo hadi sasa zaidi ya Sh.Bilioni 1.07 zimetolewa.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara hiyo Naibu Waziri Mwinjuma amesema amefurahi kufanya ziara hiyo kwani ni miongoni mwa ziara alizozifuahia zaidi kwa sababu kazi za utamaduni na Sanaa ambazo ameziona tangu amefika amevutiwa navyo vikiwemo vifaa vinavyotumika kufundishia wanafunzi.

“Vifaa ambavyo vinatumika kufundishia hatusemi haviwezi kutuzalishia watu tunawaowahitaji kwenye utamaduni na Sanaa lakini nafikiri nguvu kubwa inahitajika kuongezeka, na hicho ndicho nimekuja kukiangalia, tumekaa na kujadiliana na Mkuu wa taasisi kwa muda na tumejadiliana namna ya kustawisha mafunzo yanayotolewa

“Na hili la vifaa ni miongoni mwa mambo tuliyojadili kwa hiyo ni mambo ambayo nimepita niyaone kwa macho yangu kwasababu nimepanga kuyafanyia kazi kwa kiwango kikubwa,tunataka kuzalisha mameneja kwa ajili ya muziki , waongoza filamu, watengeneza filamu, waigizaji na vyote hivi vinahitaji vifaa na miundombinu inayoeleweka ili tupate watu wanaoweza kushindana na kasi ya Sanaa na utamaduni.

“Ujumbe wangu kwa (TaSUBa),tunatamani watu wote wanaofanya shughuli za utamaduni na Sanaa wawe wanaokaa maofisini ,wakufunzi,waigizaji,wanamuziki waone fahari kupita TaSUBa na kwa hivyo sisi tunachakata hapa namna ambavyo tutafanya taasisi hiii iingiliane kabisa na kiwanda cha muziki na filamu ambacho tunakifanya sasa hivi kwa mfano ili iwe sehemu ya mafanikio ya filamu na mziki wa nchi hii,”amesema.

Kuhusu fedha za mikopo, Naibu Waziri Mwinjuma amesema mfuko wa utamaduni na Sanaa haukulenga wasanii peke yake ,kwa hiyo sio waigizaji na wanamuziki peke yao bali watu wote ambao wanaweza kujihusisha na shughuli za Sanaa wanaweza kukopeshwa ilimradi miradi yao inamashiko.

“Kwasababu wanaokopeshwa hayakopeshwi majina bali inakopeshwa miradi ya utamaduni na sanaa na Mfuko umeshatoa Sh. Bilioni 1.07 mpaka sasa hivi na sisi hapa tunahangaika kuupatia fedha zaidi ili watu wengi zaidi wanaofanya shughuli za utamaduni na Sanaa wafaidike.

“Na lengo hasa lilikuwa na watu wengi wanaojishughulisha na shughuli hizi mtaani ambao wana mawazo makubwa lakini na unayaona kabisa haya mbele yanaenda kugeuka kuwa fedha lakini hawana Mitaji kwa ajili ya kufanyia kazi hayo mawazo yao.

“Kwa hivyo mama Samia akaona kwamba vijana wangu wanahitaji kuungwa mkono , tunashukuru sana Rais kwa jambo hili, ni miongoni mwa mambo makubwa kabisa yaliyotokea kwenye utamaduni na Sanaa toka mimi nianze kukumbuka kwamba fedha moja kwa moja fanyieni kazi mawazo yenu igeuke miradi na muingize kipato.

“Sikumbuki kama nimewahi kusoma au kuona sehemu nyingine kwamba kuna nchi Rais amefanya kama alivyofanya Rais Samia Suluhu ya kutoa fedha moja kwa moja kwa watu wanaojishughulisha na shughuli hizi ili watekeleze mawazo yao.”

Ameongeza kwa hivyo lengo ni kupandisha viwango, kuhakikisha mawazo kwenye vichwa vyetu yanafanyika lakini yanafanyika watu wakiwa huru,wakiwa na fedha.”Wanaokopeshwa wanapewa na muda wa kurudisha fedha, ambapo mradi utakuwa umekamilika na umeshaanza kutoa fedha.

“Kwa hiyo mimi nimshukuru Rais kwa kutuanzishia mfuko huu ambao ulijifia zake muda mrefu uliopita ,tunamshukuru sana lakini niwaombe wasanii na makundi mengine ambayo yanafaidishwa na mfuko huu kuhahakikisha wanapeleka miradi ya kweli inayoeleweka na wanafanya marejesho ili iweze kunufaisha wengi zaidi ambao wanajihusisha na shughuli hizo na wanahitaji mitaji.”

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Hamis Mwinjuma maarufu kwa jina la Mwana FA akisaliamiana na mwenyeji wake Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kufanya ziara ya kutembelea na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika ndani ya taasisi hiyo,Bagamoyo mkoani Pwani. PICHA ZOTE NA MICHUZI JR

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Hamis Mwinjuma akitambulishwa kwa wenyeji wa taasisi hiyo

 

About the author

mzalendoeditor