Featured Kitaifa

DKT.SHEKALAGHE:WAUGUZI NA WAKUNGA NI TASWIRA MUHIMU SEKTA YA AFYA KATIKA KUHUDUMIA WAGONJWA.

Written by mzalendoeditor

Na.Elimu ya Afya kwa Umma.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt.Seif Shekalaghe amesema watumishi wote sekta ya afya hususan wauguzi ni watu na taswira muhimu kwa sekta ya afya katika kuhudumia wagonjwa hivyo amehimiza kuzingatia maadili katika utumishi wao.

Dkt.Shekalaghe amebainisha hayo leo Machi.13.2023 jijini Dodoma katika ufunguzi wa mkutano wa jukwaa la Wauguzi na Wakunga viongozi hapa nchini ulioandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI .

Dkt. Shekalaghe amesema watumishi wote sekta ya Afya wana mchango mkubwa katika kuwahudumia wananchi hivyo kuna mchango mkubwa kuweka nguvu za pamoja katika utoaji wa huduma bora.

“Hakuna mtu yeyote anayejihisi kuona yeye ni bora kuwahudumia wagonjwa kuliko wengine, mgonjwa anaanzia getini kupima anapataje huduma hivyo ninyi nyote ni taswira muhimu katika sekta ya afya katika kuwahudumia wagonjwa fanyeni kazi kwa kuzingatia maadili” amesema Dkt.Shegalaghe.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amewakumbusha wauguzi na wakunga kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa wananchi(Customer Care) kwani ndio kipimo cha msingi kwa mteja.

“Kazi mnayofanya ni ibada hivyo ni muhimu sana kuzingatia na kujipima ubora wa huduma unayotoa , unaweza ukafanikiwa kwa vitu vingi sana kwa sababu wagonjwa unaowahudumia wanakuombea kwa mwenyezi Mungu,narudia kuwakumbusha ninyi ni jeshi kubwa na mnaotoa taswira kubwa kwa sekta ya afya”amesema.

Kuhusu utoaji wa huduma Dkt.Shekalaghe amewataka Wauguzi na Wakunga Viongozi kutoa huduma kwa upendo kwani kuna matokeo makubwa katika sekta ya Afya.

“Upendo unasaidia sana kujenga umoja kwani mgonjwa anapohitaji huduma hasaidiwi na mtoa huduma mmoja tu,hivyo ninyi mnapokuwa na upendo ninyi kwa ninyi lazima huduma inakuwa bora, na penye uongozi mzuri pana mabadiliko”amesisitiza.

Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Serikali Ziada Sellah amesema katika mkutano huo utasaidia kuweka mikakati endelevu katika uboreshaji wa huduma za Afya katika ngazi zote na kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo uongozi na kujadili changamoto mbalimbazi zinazowakumba wauguzi.

“Tutatumia mkutano huu kujadili mambo mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma zenye staha, zinazojali utu, heshima na upendo ikiwemo maadili na Customer Care(ubora wa huduma)”amesema.

Ikumbukwe kuwa, Mkutano wa Wauguzi na Wakunga Viongozi umeanza leo Machi.13-17/2023 na unahusisha wauguzi kutoka Hospitali ya Taifa, Hospitali ya Kanda, Hospitali za Rufaa za mikoa, Hospitali Maalum, Wauguzi Wakuu wa Mikoa, Wauguzi Wakuu wa Halmashauri lengo ni kuwajengea uwezo katika masuala ya uongozi na Usimamizi wa Huduma za Afya ili waweze kusimamia na na kuimarisha utoaji wa Huduma bora za Afya ambapo umekwenda sambamba na kaulimbiu isemayo ‘’ Mchango wa Wauguzi na Wakunga ni Muhimu katika Kuimarisha Utoaji wa Huduma Bora za Afya nchini”

About the author

mzalendoeditor