Featured Kitaifa

REA WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA KUIGUSA JAMII

Written by mzalendoeditor

Wafanyakazi Wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiwa wamejipanga tayari kwa maandamano katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika ngazi ya Mkoa, wilayani Kondoa mkoani Dodoma, Machi 8, 2023. Kulia (mwenye kofia) ni Mtaalamu wa Jinsia na Nishati – REA, Dkt. Joseph Sambali.

Baadhi ya Wafanyakazi Wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi kabla ya kuelekea katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika ngazi ya Mkoa, wilayani Kondoa mkoani Dodoma, Machi 8, 2023.

Wafanyakazi Wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiandamana wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika ngazi ya Mkoa, wilayani Kondoa mkoani Dodoma, Machi 8, 2023.

Baadhi ya Wafanyakazi Wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiwa katika picha ya pamoja na Mtaalamu wa Jinsia na Nishati – REA, Dkt. Joseph Sambali (katikati-waliosimama), muda mfupi kabla ya kuelekea katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika ngazi ya Mkoa, wilayani Kondoa mkoani Dodoma, Machi 8, 2023.

Veronica Simba – REA

Wafanyakazi wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuungana na wanawake wengine kutoka Taasisi za Serikali na Binafsi katika maadhimisho ngazi ya Mkoa, yaliyofanyika wilayani Kondoa mkoani humo.

Pamoja na kushiriki sherehe hizo zilizofanyika leo Machi 8, 2023 Mgeni Rasmi akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Wanawake wa REA wameadhimisha pia Siku ya Wanawake Duniani kwa kuigusa jamii.

Akizungumzia ushiriki wa REA katika Maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Wanawake, Tawi la REA, Wilhelmina Cheyo amesema azma yao ya ushiriki wenye tija imetimia.

Akifafanua, Cheyo amesema wanawake wa REA walipanga kuadhimisha siku hiyo kwa kuigusa jamii, jambo ambalo wamelitimiza kwa kununua na kugawa majiko banifu na ya gesi pamoja na mitungi yake kwa wanufaika 125 kutoka vijiji vya Zanka na Kigwe wilayani Bahi.

“Kwakweli tunamshukuru sana Mungu kutuwezesha kutimiza azma yetu. Hatukutaka ushiriki wetu uishie kwenye kuandamana tu na kusherehekea bali uwe ushiriki wenye tija kwa kuigusa jamii hasa akina mama wenzetu wahitaji,” amesisitiza.

Akieleza zaidi, Mwenyekiti amesema hafla ya kugawa majiko ilifanyika Machi 6, 2023 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Godwin Gondwe.

Ameongeza kuwa Umoja wa Wafanyakazi Wanawake Tawi la REA una malengo makubwa ambayo wanaamini wataendelea kuyatimiza mwaka hadi mwaka kwa kuigusa jamii ya wanawake hasa waishio vijijini ambao wengi wao huishi katika mazingira magumu.

Aidha, amefafanua zaidi kuwa dhamira ya kuwalenga wanawake waishio vijijini inatokana pia na mwelekeo wa kazi wa REA ambayo inahusika na upelekaji nishati safi na salama vijijini.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka huu ni Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia Chachu katika kuleta Usawa wa Kijinsia.

About the author

mzalendoeditor