Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wadau wa zao la Chikichi kuhusu mafanikio ya mpango mkakati wa kufufua, kupanua na kuendeleza zao la chikichi nchini, kwenye ukumbi wa NSSF, Kigoma Februari 26, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde akizungumza na wadau wa zao la chikichi kwenye kikao kilichoongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwenye ukumbi wa NSSF, Kigoma Februari 26, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wa vyama vya siasa watumie majukwaa waliyonayo kuhimiza kilimo cha michikichi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.
“Viongozi wote wa Mikoa, Wilaya, na wa vyama vya siasa mnayo majukwaa ya kukutana na wananchi kila wakati. Twendeni tukahamasishe wananchi walime michikichi kwa sababu ni zao litakalowapatia fedha kwa muda mrefu,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumapili, Februari 26, 2023) wakati akizungumza na wadau wa zao la chikichi mkoani Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF. Wadau hao wanajumuisha wakulima, wazalishaji miche, wakamuaji mawese, viongozi wa vijiji, viongozi wa taasisi za fedha, viongozi wa wilaya, Halmashauri na mkoa.
Waziri Mkuu ameitisha kikao hicho ili kujadili changamoto zinalolikabili zao hilo na kujadiliana njia za kuliendeleza ili kuhakikisha nchi inakuwa na kiasi cha kutosha cha mafuta ya mawese, hatua ambayo amesema itasaidia nchi kuepuka kuagiza kiasi kikubwa cha mafuta kutoka nje nchi.
Amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wenye ardhi inayokubali zao hilo wafanye hivyo mara moja kwani mbali na kuwapa fedha za uhakika, litaleta fursa ya ajira kupitia viwanda vinavyofunguliwa.
“Chikichi ni fursa, chikichi ni maendeleo, Ni fursa ya kuleta viwanda hapa Kigoma na kwenye mikoa mingine itakayolima zao hili. Chikichi ni uchumi, ni uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa kitaifa,” amesisitiza.
Akizungumzia kuhusu mahitaji ya mafuta ya kula nchini, Waziri Mkuu amesema: “Hivi sasa mahitaji ya mafuta nchini ni zaidi ya tani 650,000 huku uzalishaji ukikadiriwa kuwa tani 290,000 tu. Hivyo, kiasi cha tani 360,000 sawa na asilimia 55.4 huagizwa kutoka nje ya nchi na kuigharimu Serikali takribani shilingi bilioni 470 kila mwaka. Tunahitaji hii fedha iendelee kutumika nchini,” amesema.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa kufanya mageuzi makubwa katika mazao ya mafuta ikiwemo michikichi.
“Mageuzi haya yanakwenda sambamba na kupanda miche mipya iliyoboreshwa ambayo ina uzalishaji mkubwa wa mafuta. Wana-Kigoma tuamue sasa hivi tupande michikichi kwa bidii,” amesisitiza.
Serikali ilichukua hatua za makusudi za kuliingiza zao la michikichi katika orodha ya mazao ya kimkakati. Mazao mengine ya kimkakati ni pamba, tumbaku, kahawa, korosho, chai, mkonge, zabibu na alizeti.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wadau hao, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alisema hiyo inaendelea na uzalishaji wa mbegu na miche bora ya michikichi aina ya TENERA inayotoa mafuta mara tatu zaidi ya aina ya DURA ambayo inalimwa na wakulima kwa takribani asilimia 90.
“Hadi kufikia Januari, 2023 TARI Kwa kushirikiana na kampuni binafsi imezalisha jumla ya mbegu milioni 14.14. Kati ya hizi, mbegu milioni 11.59 zimezalishwa na TARI na mbegu milioni 2.54 zimezalishwa na kampuni binafsi zikiwemo FELISA, NDF na Yangu Macho Group Ltd.”
Alisema kati ya mbegu milioni 14.14 zilizozalishwa, mbegu milioni 9.60 zimekwisha sambazwa na kuoteshwa na taasisi mbalimbali zikiwemo JKT na Magereza, Halmashauri zote nane za mkoa wa Kigoma, Halmashauri 25 za nje ya mkoa wa Kigoma, vituo vya TARI na Wakala wa Mbegu za kilimo Tanzania (ASA).
Amesema hadi kufikia Januari, 2023 jumla ya miche 3,122,566 imepatikana ambapo miche 1,968,087 imegawiwa kwa wakulima ndani na nje ya mkoa wa Kigoma.
Mkutano huo wa siku moja bado unaendelea ambapo wakulima na wadau wengine wanaendelea kutoa maoni yao.