Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea nakala za Hati za Utambulisho za Balozi mteule wa Misri nchini, Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Balozi mteule wa Misri nchini, Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea nakala za Hati za Utambulisho za Balozi mteule wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimsikiliza Balozi mteule wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
…………………………….
Na.Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amepokea nakala za Hati za Utambulisho za mabalozi wateule wa nchi za Misri na Marekani.
Mhe. Waziri Tax amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi wa Misri nchini, Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail na Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle jana jioni katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mabalozi hao kwa nyakati tofauti mara baada ya kupokea nakala zao za hati za utambulisho, Dkt. Tax amewahakikishia ushirikiano kutoka Serikalini wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao hapa nchini na kuwasihi kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na nchi zao.
Balozi mteule wa Misri nchini, Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Misri na Tanzania katika sekta za nishati hususani mradi wa bwawa la mwalimu Nyerere, kilimo, biashara na uwekezaji.
“Misri na Tanzania tunayo mengi ya kushirikiana, tunaahidi kuendeleza ushirikiano wetu kwa maslahi mapana ya pande zote mbili, wakati wa utumishi wangu hapa Tanzania nitaendeleza kwa maslahi mapana ya wananchi wetu wote,” alisema Balozi Ismail
Kwa upande wake Balozi Mteule wa Marekani, Mhe. Michael Battle amesema Marekani na Tanzania zimekuwa marafiki wa muda mrefu, na itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za Utalii, Kilimo, afya, biashara na uwekezaji pamoja na sekta nyingine za kimkakati.
“Ni furaha kwangu kuwepo hapa leo na kukabidhi nakala ya hati ya utambulisho wangu hapa nchini Tanzania, napenda kuahidi kwa kipindi nitakachokuwa hapa nitahakikisha kuwa uhusiano wetu wa kidiplomasia unakuwa na kuimarika kwa maslahi ya mataifa yetu,” alisema Balozi Battle.