Featured Kitaifa

BODI MPYA CDTI YATAKIWA KUZALISHA MAAFISA WATAKAOLETA  TIJA KATIKA JAMII

Written by mzalendoeditor
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akiongea katika uzinduzi wa bodi ya uendeshaji wa chuo cha maendeleo ya jamii Tengeru.
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akikabidhi mmoja ya wajumbe wa bodi hiyo vitendea kazi.
MWENYEKITI wa Bodi ya Uendeshaji wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru John Elton, akiongea na waandishi wa habari mara baada ya bodi hiyo kuzinduliwa.
……………………………………
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA

Naibu katibu mkuu wa wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum Amon Mpanju ameitaka bodi ya uendeshaji wa chuo cha maendeleo ya jamii Tengeru (CDTI) kuhakikisha wanaboresha mafunzo ili kuweza kuzalisha maafisa watakaoenda kuleta tija katika jamii.

Mpanju ameyasema haya wakati akizindua bodi ya tatu ya uendeshaji wa chuo hicho ambapo alieleza kuwa ni ukweli usiopingika  kuna changamoto nyingi zinazoikabili jamii ikiwemo ukatili dhidi ya wanawake na watoto, wananchi kutokupenda maendeleo na kutumia fursa zinazowazunguka, kuondoa lindi la umasikini kwani zaidi ya asilimia 25 ya watanzania wanaishi chini ya lindi la umasikini.
“Ni nani anaweza kutanzua na kuhakikisha ustawi na maendeleo katika jamii, ni maafisa maendeleo ambao kitovu chao ni taasisi hii hivyo muhakikishe maafisa maendeleo wanazalishwa wenye weledi, ujuzi, maarifa na stadi za kuwezesha kutoa mchango katika utatuzi wa changamoto zinazo kabili jamii ya kitanzania na taifa kwa ujumla,”Alisema Mpanju.
Alifafanua kuwa sambamba na hayo pia bodi hiyo inalo jukumu la kusimamia nidhamu na maadili ya menejimenti na watendaji ambapo wanawatwisha mzigo mkubwa kwa niaba ya serikali na ana imani mzigo huo wataubeba vema kwasababu wanao ujuzi, maarifa, weledi na sifa zilizopitiliza kuweza kuendesha taasisi hiyo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi hiyo John Elton alisema kuwa wamejipanga kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ya kinidhamu kwa kuwaelekeza wanafunzi jinsi ya kwenda kuishi na kuwa watu wenye faida, heshima na kuhesimika  katika jamii.
Alisema kuwa namna ya kuishi ni lazima mtu awe na weledi na nidhamu na mojawapo ikiwa ni kumuheshimu binadamu mwingine na kumthamini kwani bado wanakazi ya kuwafundisha wanachuo na kuangalia kwamba ni nini makosa ya kinidhamu kutokea.
Aidha kwa upande wa ajira alisema kuwa kutokana na changamoto ya ukosefu wa ajira wamejipanga kila kijana atakapohitimu katika chuo hicho,  yeye mwenyewe awe ni chanzo cha ajira na kwenda kusaidia  jamii kuleta maendeleo kwani maendeleo sio kwenda kutegemea ajira ya kukaa ofisini.
“Tunataka wakabuni ajira zinazoweza kuleta chakula, kuratibu jamii na kuhakikisha kwamba miundombinu ambayo imewekwa na serikali kwa gharama nyingi inalindwa na inatunzwa kwa nidhamu kubwa ikiwemo kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa, mazingira pamoja na kuunda  vikundi vyenye tija kwaajili ya kuleta maendeleo,” alisema.

About the author

mzalendoeditor