Kiongozi wa Mradi wa Afya –Tek Dkt.Angel Dillip akiwasilisha mada namna wanavyotekeleza mradi wa Afya -Tek katika halmashauri na Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani.
Afisa Programu ,Elimu ya Afya kwa Umma,Wizara ya Afya Simon Nzilibili akizungumza katika hafla ya kutembelea mradi wa Afya Tek na Usimamizi Shirikishi juu ya Masuala ya Afya katika halmashauri na Manispaa ya Kibaha.
Msajili wa Baraza la Famasi Tanzania Elizabeth Shekalaghe akichangia mada katika kikao cha mradi wa Afya -Tek Kibaha Pwani.
Afisa Ufuatiiaji na Tathmini Elimu ya Afya kwa Umma ,Idara ya Kinga ,Wizara ya Afya Erick Msunyaro akichangia mada katika kikao cha mradi wa Afya -Tek Kibaha Pwani.
Afisa Tehama Elimu ya Afya kwa Umma ,Idara ya Kinga ,Wizara ya Afya Victor Kisila akiwa katika kikao cha mradi wa Afya -Tek Kibaha Pwani.
Happiness Ndelwa Mratibu wa Afya ngazi ya Jamii Halmashauri ya Kibaha akichangia mada kikao cha Afya -Tek Kibaha Pwani
……………………………….
Na.Faustine Gimu,Elimu ya Afya kwa Umma,Wizara ya Afya.
Katika kuelekea Bima sheria ya Bima ya Afya kwa Wote,wadau wa sekta ya Afya wameaswa kushirikiana na Serikali uimarishaji wa mifumo katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya.
Hayo yamebainishwa Wilayani Kibaha Mkoani Pwani na Afisa Programu ,Elimu ya Afya kwa Umma,Wizara ya Afya Simon Nzilibili katika hafla ya kutembelea mradi wa Afya Tek na Usimamizi Shirikishi juu ya Masuala ya Afya katika halmashauri na Manispaa ya Kibaha.
“Tunapoelekea Bima ya Afya kwa Wote,tunatoa wito wadau wetu wanaotekeleza mradi wa Afya –Tek wawe tayari ,pale inapotokea serikali inahitisha wadau mbalimbali walio na utaalam kwenye matumizi ya mifumo tuweze kushirikiana kwa pamoja ili kuboresha na itarahisisha wananchi kunufaika zaidi na Bima ya Afya kwa Wote kupitia Mifumo iliyo imara”amesema.
Katika hatua nyingine Nzilibili ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kwa kuwa mstari wa mbele katika usimamizi kuhakikisha Elimu ya Afya kwa Umma inamfikia kila mtu hususan elimu katika kuelekea Bima ya Afya kwa Wote na kuongeza kuwa wataendelea kushirikiana na wadau katika uimarishaji wa huduma za Afya.
Kiongozi wa Mradi wa Afya –Tek Dkt.Angel Dillip amesema lengo kuu la Mradi wa Afya-Tek ni kusaidia kuboresha afya ya mama,mtoto na vijana balehe ambapo hadi sasa wameshafikiwa wanajamii 230,000 sawa na asilimia 92% ya idadi ya wanajamii wote katika halmashuri ya Wilaya ya Kibaha na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.
“Tumefikia wanajamii laki mbili na elfu thelathini(230,000]sawa na asilimia 92% na faida za Afya –Tek imeweza kupunguza kuchelewa kuhudumia wagonjwa na mgonjwa anapofika zahanati au kituo cha Afya ufuatiliaji unafanyika kwa uharaka na kuweza kupata huduma kwani kabla ya Afya –Tek kulikuwa na njia za utumiaji wa karatasi na ilikuwa vigumu kufuatilia wagonjwa kwamba wamefika kituo cha afya au la lakini kwa kutumia mfumo wa Afya-Tek huduma inafanyika kwa uharaka na Mgonjwa anapata huduma”amesema.
Mganga Mkuu Halmashauri ya Kibaha Mkoani Pwani Dkt.Wilford Kondo amesema mradi wa Afya-Tek umeweza kusaidia kupunguza kutoka vifo 8 vya mama wajawazito mwaka 2021 hadi kifo kimoja kwa mwaka 2022 huku mwaka huu hakuna kifo kilichoripotiwa katika halmashauri hiyo huku mwakilishi Baraza la Famasi Kibaha Wilbard Semvua akisema mfumo wa Afya Tek unarahisisha mgonjwa kupata huduma kwa wakati.
Mtoa huduma wa duka la dawa Muhimu Daima Gada pamoja na mtoa huduma ya Afya ngazi ya jamii kata ya Kongowe Simen Rashid wamesema Afya –Tek imerahishisha kuokoa muda pindi wanapotoa huduma na kuibua changamoto zinazotokea.
Ikumbukwe kuwa Mradi wa Afya-Tek unatekelezwa katika Halmashauri ya Kibaha na Manispaa ya Kibaha lengo likiwa ni kuchangia kupunguza vifo vya wajawazito,mama waliojifungua, na watoto chini ya miaka mitano na kuboresha afya za vijana balehe ambapo unatekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya,TAMISEMI,Baraza la Famasi,Timu za Afya za Mkoa na Halmashauri na Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Apotheker na D-tree International .
Hivyo,mradi huu hutumia mfumo wa teknolojia ya kidijitali kuwaunganisha watoa huduma za afya katika ngazi ya jamii(WAJA),wahudumu wa maduka ya dawa muhimu(DLDM) na vituo vya huduma za afya na umeanza kutumika kuanzia Julai 2020 na hadi sasa umeunganisha watoa huduma ngazi ya Jamii 240,DLDM 149, vituo vya kutolea huduma za afya vya umma 39 na binafsi 10 .
Pia ,mradi huu ulitoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo takribani 500 ,vitendea kazi ikiwemo simu za mkononi 450 zenye mfumo wa Afya Tek.