WATU 17 wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia leo Jumamosi Februari 4, 2023 wilayani Korogwe mkoani Tanga.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba leo imeeleza kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na kusababisha vifo vya watu 17 na Majeruhi 12.
Ajali hiyo imetokea usiku katika eneo la Magira Gereza Kata ya Magira Gereza Tarafa ya Mombo wilayani Korogwe, barabara ya Segera – Buiko.
“Ajali hii imesababisha vifo 17 na majeruhi 12 ambao majina yao wote hayajafahamika, miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Korogwe na majeruhi 10 wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo na majeruhi wawili wamebaki Hospitali ya Korogwe kwa matibabu.
“Ajali hii imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso na Coaster iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu na abiria 26 ikitokea Dar kwenda Moshi kwenye mazishi” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imetaja chanjo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi na uzembe wa dereva fuso kulipita gari la mbele bila ya kuchukua tahadhari na kugongana na Coaster.
CHANZO:MWANANCHI.CO.TZ