Featured Kitaifa

TANZANIA NA FINLAND ZAAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA BIASHARA

Written by mzalendoeditor

Serikali za Tanzania na
Finland zimeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta zenye maslahi
mapana ya kiuchumi kwa wananchi wa nchi hizi mbili ikiwemo biashara, utalii na
uwekezaji.

Ahadi hiyo imetolewa katika
mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Uchumi wa Finland, Mhe. Mika
Lintilä walipokutana katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 31
Januari 2023.

Katika mazungumzo hayo
viongozi hao wamejadili juu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara,
uwekezaji, utalii, teknolojia ya habari na mawasiliano, usafirishaji, afya,
kilimo, madini, nishati, elimu, mazingira na tafiti ili kupitia sekta hizo
wananchi hususan wa Tanzania wanufaike kiuchumi na kijamii.

Dkt. Tax ameeleza kuwa
amefurahishwa na ziara ya Mhe. Mika Lintilä na ujumbe wake
nchini ikiwemo ujumbe wa wafanyabiashara alioambatana nao kutoka katika sekta
za msingi kwa maendeleo ya pande zote mbili.

“Tanzania na Finland zina
ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa kati ya nchi hizo mara baada ya uhuru wa
Tanganyika mwaka 1962. Tupo tayari kuendelea kushirikiana na Finland katika
kujenga uchumi wa kidigitali ili kuyafikia mapinduzi ya viwanda” alisema Dkt.
Tax.

Vile vile, ametumia nafasi
hiyo kuishukuru Serikali ya Finland kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 19 wa Nchi
za Nordic na Afrika uliofanyika mwezi Juni 2022. Pia ameeleza kuwa Tanzania
itaendelea kushiriki kwenye majukwaa mbalimbali ili kuwasilisha mchango wake
katika masuala ya kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake, Mhe. Mika
Lintilä ameeleza kuwa Umoja wa Ulaya umetenga fedha kiasi cha Euro
Billioni 300 kwa ajili ya kushirikiana na nchi zinazoendelea na zile za Kusini
mwa Jangwa la Sahara katika sekta za maendeleo.

Vile vile, ameongeza kuwa
tarehe 23 na 24 Februari 2023 kampuni za biashara zipatazo 40 kutoka
Finland zitashiriki katika Jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Umoja wa
Ulaya litakalofanyika jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo,
Waziri Lintilä amekutana na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ambapo viongozi hao wamekubaliana kuimarisha
ushirikiano katika masuala ya biashara na uwekezaji ili kukuza uwiano wa
biashara kati ya nchi hizi mbili ambao bado ni mdogo.

Pia Dkt. Kijaji ameongeza
kuwa, Tanzania itaendelea  kuongeza samani ya bidhaa zake kama mbao,
chakula na madini ili kuziwezesha kuingia katika soko la kimataifa ikiwemo
Finland.

Waziri Lintilä yupo
nchini kwa ziara ya siku nne (4) ambapo ameambatana na kundi la wafanyabiashara
wapatao 18 kutoka katika sekta mbalimbali za kiuchumi ili kujionea maeneo
mbalimbali ya uwekezaji  na biashara.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kati)akizungumza na Waziri wa Uchumi wa Finland, Mhe. Mika Lintilä (hayupo pichani)  katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 31 Januari 2023. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na kulia ni Afisa Mambo ya Nje, Bw. Albert Philip.

 

Waziri wa Uchumi wa Finland, Mhe. Mika Lintilä (kulia) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (hayupo pichani) katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 31 Januari 2023. Pembeni ya Mhe. Lintilä ni Balozi wa Finland nchini, Mhe. Theresa Zitting.

Mazungumzo yakiendelea.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akisalimiana na Waziri wa Uchumi wa Finland, Mhe. Mika Lintilä alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 31 Januari 2023. 

Dkt. Tax akimkabidhi zawadi Mhe.Mika Lintilä

About the author

mzalendoeditor