Featured Kitaifa

MASHIRIKIANO YANAHITAJIKA KUPAMBANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI – MHE. OTHMAN.

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuwa tishio na changamoto kubwa hapa Visiwani, kutokana na athari za moja kwa moja katika maisha ya wananchi.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo huko Ofisini kwake Migombani Zanzibar, akiongea na Naibu Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Bw. Rick Shearn, kuhusu masuala mbalimbali ya Mazingira, ushirikiano, uchumi, jamii na maendeleo.

Amesema kuwa, tishio na changamoto zaidi za mabadiliko ya tabianchi, zinadhihiri katika mwenendo mzima wa maisha ya kawaida ya wananchi na hasa wanaoishi katika Ukanda wa Pwani, ambako kwa kiasi kikubwa kumebainika athari za waziwazi.

Akitaja viashiria vya athari hizo, Mheshimiwa Othman ameeleza hali ya maeneo mengi ya visiwa vya Zanzibar, yakiwemo ya kilimo na makaazi ya watu, kuvamiwa na maji chumvi, na hivyo kudhoofisha mavuno, kipato cha wananchi, na hatimaye kuyumba kwa uchumi, kuanzia kwa mtu binafsi, familia na ikibidi hata pato la Nchi.

“Bila shaka juhudi kubwa zinahitajika na mashirikiano ya pamoja ili kunusuru hali hiyo isiendelee, kwani inaathiri hata Mipango ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwemo utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu”, amesema Mheshimiwa Othman.

Aidha Mheshimiwa Othman ameeleza matumaini ya Zanzibar kupitia mahusiano mema na Jamii ya Kimataifa, katika kukabiliana na athari za tishio hilo kwa haraka, hasa wakati huu ambao mazingira ya kisiasa nchini yameanza kufunguka, sambamba na juhudi za kuendeleza maridhiano kufuatia uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) hapa Visiwani.

Naye Balozi Shearn, kwa upande wake amesema kwamba Nchi yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika utekelelezaji wa mikakati muhimu ya kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi, ili hali hiyo ambayo kwa sasa ni tatizo la ulimwengu, isiendelee kuleta athari zaidi.

Balozi Shearn amesisitiza haja ya kuendelea na ujenzi wa demokrasia, utawala wa sheria na maridhiano ya kisiasa, ili kuweka mazingira bora yatakayopelekea fursa nyingi za kujiletea maendeleo na hatimaye kuijenga Nchi kiuchumi.

Katika Msafara wake, Balozi Shearn aliambatana na Maafisa mbalimbali kutoka Ubalozi wa Uingereza Nchini Tanzania akiwemo Mkuu wa Masuala ya Mazingira na Tabianchi, Bi Catherine Pye.

 

About the author

mzalendoeditor