Featured Kitaifa

MKOA WA SINGIDA KUNUFAIKA NA MRADI WA BILIONI 7 KUPITIA AWAMU YA TATU YA MRADI WA REA WA PERI URBAN

Written by mzalendoeditor

 

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Mhandisi Pasikasi Muragili (katikati) akiwa pamoja Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Singida (waliokaa kushoto) na ujumbe wa Wakala wa Nishati Vijijini – REA  (waliokaa kulia) wakati wa kikao cha kumkabidhi Mkandarasi  Central Electrical International Ltd anayetekeleza  Mradi wa Kusambaza Umeme katika Maeneo ya Vijiji Miji katika mkoa wa Singida.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera Mipango na Utafiti wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Nicolaus Moshi akizungumza wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi Mradi wa Kusambaza Umeme katika Maeneo ya Vijiji Miji katika kitongoji cha Kitope Darajani kilichopo Wilaya ya Singida mkoa humo.

Utambulisho wa Wafanyakazi wa Kampuni ya Central Electrical International Ltd watakaojenga Mradi wa Kusambaza Umeme katika Maeneo ya Vijiji Miji katika Mkoa wa Singida.

Mkuu wa Wilaya Singida, Mhe. Mhandisi Pasikasi Muragili (aliyesimama) akihutubia Wananchi wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme katika Maeneo ya Vijiji Miji katika Mkoa wa Singida katika kitongoji cha Kitope Darajani Kaya ya Mwankoko Wilaya ya Singida hivi karibuni.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Mhandisi Pasikasi Muragili akiwasha king’ora kuashiria kuzindua Mradi wa Kusambaza Umeme katika Maeneo ya Vijiji Miji katika Mkoa wa Singida.

Picha ya pamoja ya Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Singida pamoja na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), REA na Mkandarasi baada ya uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme katika Maeneo ya Vijiji Miji katika Mkoa wa Singida.

Picha ya pamoja ya viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM), REA na Mkandarasi baada ya uzinduzi wa Mradi wa Mradi wa Kusambaza Umeme katika Maeneo ya Vijiji Miji katika Mkoa wa Singida.

…………………..

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Mhandisi, Pasikasi Muragili hivi karibuni alishuhudia tukio la Mkandarasi (Kampuni ya Centre Electrical International Ltd) kukabidhiwa rasmi Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye maeneo yenye sifa za vijiji ingawa yapo mjini (PERI Urban III) Singida mjini; Mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 7.1.

Katika hafla hiyo; Mhandisi Muragili alisema vijiji na vitongoji vyote vya Manispaa ya Singida ambavyo havikuwa vikipata huduma ya nishati ya umeme, sasa vimepata nishati hiyo kupitia Mradi huo wa PERI Urban Awamu ya Tatu.

Tukio lililofanyika katika kitongoji cha Kitope Darajani katika Manispaa ya Singida ambapo Mhandisi Muragili alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa Singida, Mhe. Peter Serukamba na kuwataka Wananchi wa Manispaa ya Singida kuibua shughuli za kiuchumi ili watumie nishati ya umeme kujiongezea kipato.

“Anzeni sasa kujiunganishia huduma ya umeme (Wiring) ili tuinue uchumi wa Watu, kwa kuanza kuibua shughuli za kiuchumi ambazo zinatumia nishati ya umeme kama viwanda vidogo vidogo” alisema.

Aidha, Mhandisi Muragili alipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa jitihada za kusambaza umeme vijijini na alimtaka Mwakilishi wa Kampuni ya Central Electrical International Limited kutekeleza mradi huo kwa weledi na ufanisi wa kiwango cha juu.

Akizungumza kwa niaba ya Wananchi, Diwani wa Kata ya Mwamkoko, Mhe. Emmanuel Kiema aliahidi kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi na kuwataka Wananchi kulinda miundombinu ya kusambaza umeme.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijni (REA); Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sera, Mipango na Utafiti, Nicolaus Moshi alisema Mradi huo utatekelezwa kwa miezi 18 ambapo utanufaisha mitaa 34 iliyopo kwenye kata tisa na kuunganisha Wateja wa awali 1,802 kwa gharama za shilingi bilioni 7.1

Moshi alimtaka Mkandarasi kuzingatia mahusiano mazuri na Viongozi na Wananchi katika eneo la utekelezaji wa Mradi huo pamoja kumtaka azingatie muda wa utekelezaji wa mkataba kwa kuwa hakutakuwa na nyongeza. 

About the author

mzalendoeditor