Featured Kitaifa

ASKOFU MSIMBE:VIJANA JIEPUSHENI NA TAMAA YA MWILI,MALI NA MADARAKA

Written by mzalendoeditor
Washiriki wa Kongamano la 14 la TMCS Kitaifa kutoka katika Kanda mbalimbali za Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki wanasoma Vyuo na Vyuo Vikuu nchini,wakiwa kwenye Semina katika Kongamano linaloendelea katika Viwanja vya Shule ya Wasichana Marian Bagamoyo Jimboni Morogoro.(Picha na Ndahani Lugunya)
…………………………….
Na Ndahani Lugunya-Bagamoyo.
Askofu wa Jimbo  Katoliki la Morogoro Mhashamu Lazarus Vitalis Msimbe SDS amewataka vijana kuepuka tamaa za mwili,mali na madaraka katika maisha yao kwani wasipoweza kuzitawala tamaa hizo zinaweza kuwaletea matatizo wao wenyewe na kwa watu wengine.
Amesema hayo wakati akitoa homilia yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu Kumbukumbu ya Watoto Mashahidi, ikiwa ni siku ya pili ya mwendelezo wa Kongamano  la 14 la TMCS Kitaifa,linaloendelea kufanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian-Bagamoyo Jimbo Katoliki la Morogoro.
Katika homilia yake Askofu Msimbe amesema kwamba katika suala la tamaa za mali wapo baadhi ya watu wanadhubutu hata kutoa uhai wa wengine  kwa sababu ya kutaka mali,vivyo hivyo na kwa upande wa tamaa za mwili pia zinawafanya watu watende dhambi nyingi.
Katika tamaa ya madaraka amesema kwamba  wapo watu wanaotamani madaraka kiasi cha kuwa tayari kusababisha vita ili kusudi watu waangamie kwa sababu ya wao kutaka kuwa viongozi na madaraka na hicho ni kishawishi kikubwa cha watu waliowengi duniani,na kwa hivyo vijana wajitahidi kuepa tamaa hii popote pale wanapokuepo.
“Tamaa hizo tatu zinamsumbua sana binadamu na anaangukia katika dhambi nyingi kwa sababu ya tamaa za mwili,mali na madaraka kama ilivyokuwa kwa Herode ambaye aliona atapoteza madaraka yake kwa kumhofia mtoto Yesu mfalme aliyezaliwa kiasi cha kuua watoto wengi wasiokuwa na hatia.
Kwa hiyo vijana mjifunze namna ya kutawala hizo tamaa tatu ambazo kila mmoja anaweza kuzipata kwa wakati wake.tuzitawale hizo tamaa za mali,mwili na madaraka  ili tuweze kuwa na maisha adilifu,” amesema Askofu Msimbe.
Katika hatua nyingine amesema kwamba thamani yamaisha haipo katika wingi wa maisha atakayoishi mwanadamu,bali kile anachokifanya ndicho kinachoweza kumpa  thamani hata kama ataishi maisha mafupi,kumbe vijana wajifunze kusimamia bila woga yale wanayo yaamini.
“Kwa hiyo vijana tujifunze kusimamia yale tunayo yaamini na kuyaelewa kwamba ni ya kweli na ni ya maana  katika maisha.tusimame bila woga.ndiyo mwaliko kwenu vijana kusimamia yale unayo yaamini na kuyasemea bila woga na bila kuzunguka zunguka kwani ukweli ndio utakao kuletea uhuru.
Uhuru wa kweli unapatikana katika kuwa mkweli  kwako kwa wenzako na kwa Mwenyezi Mungu.hivyo vijana msimamie yale mnayo yaamini kuwa ni ya kweli.vijana mjivunie imani yenu na kwa hivyo muonyeshe kweli kwa vitendo kwa kuyasimamia yale ambayo mna yaamini kuwa ni ya kweli,” amesisitiza Askofu Msimbe.
Askofu Msimbe ameendelea kusema kwamba kijana Mkatoliki atakapojivunia imani yake atakuwa tayari kuitetea,kuilinda na kuineza kwa wengine wasio ijua.
“Wito na mwaliko wangu kwenu vijana mjivunie imani yenu kwa sababu ndiyo wakati huu wa ujana wakujivinia imani yako, ndiyo wakati huu wa ujana wa kupanda mbegu ya imani ambayo itaota na kushika mizizi utakapokuwa mtu mzima tayari hakuna mtu atakaye kuyumbisha kwa sababu wewe utakuwa na misimamo mizuri.
Wakati huu wa ujana ndiyo wa kutengeneza  maisha ya kitakatifu kwani thamani yako wewe haiko katika kuishi miaka mingi  kwa sababu hata katika umri huu wa ujana  unaweza kufanya mambo mengi na ya ajabu  kwani wapo Watakatifu wengi vijana,”amesema Askofu Msimbe.
Pamoja na hayo Askofu Msimbe amewasisitiza vijana kuona umuhimu wa Sakramenti ya kitubio,kwani wengi wao wanatenda dhambi lakini wanaendelea kubaki nazo na kuchukulia kama jambo la kawaida.
Askofu Msimbe amehitimisha homilia yake kwa kuwaalika  vijana hao kutumia fursa ya uwepo wao  Bagamoyo mlango wa imani kufanya hija katika maeneo ya hija,ili kusali,kufanya toba,kumsifu na kumshukuru Mungu.
“Mtumie nafasi hii nzuri  ya ujio wenu hapa Bagamoyo  ambayo ni sehemu ya kihistoria kiimani ambapo Ukristo umeanzia hapa.wamisionari wa kwanza waliingia hapa na kwakupitia kwao dini yetu katoliki ikaanzia hapa,” amesema Askofu Msimbe.

About the author

mzalendoeditor