Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU AAGIZA WAKUU WA WILAYA KUKUTANA NA WAFUGAJI

Written by mzalendoeditor

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao cha pamoja na Mawaziri wa Kisekta, Makatibu Wakuu na  Naibu Makatibu Wakuu, Kamati za  Ulinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya za  Morogoro cha  kujadili changamoto za usimamizi wa ardhi ndani ya mkoa  huo, kwenye ukumbi wa Magadu katika Manispaa ya Morogoro,

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao cha pamoja na Mawaziri wa Kisekta, Makatibu Wakuu na  Naibu Makatibu Wakuu, Kamati za  Ulinzi na Usalama za Mkoa na wilaya za Morogoro cha  kujadili changamoto za usimamizi wa ardhi ndani ya mkoa  huo kwenye ukumbi wa Magadu katika Manispaa ya Morogoro, Disemba 24, 2022.  Kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki na kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Angela Kairuki. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

…………………………

*Pia asisitiza vikao vya pamoja vya maridhiano ya wakulima na wafugaji

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza Wakuu wa Wilaya kuitisha vikao na wafugaji ili kujadiliana na kuweka namna bora ya kufanya shughuli za ufugaji ikiwa ni pamoja na kutambua mifugo yote iliyoko ndani ya Wilaya husika na kuweka zuio la mifugo mingine kuingizwa katika wilaya zao.

Mheshimiwa Majaliwa pia ameagiza viongozi katika mikoa na wilaya kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo yote yenye wafugaji na wakulima ambapo pia kuna vyanzo vya maji.

Amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona uharibu wa vyanzo vyote vya maji vinadhibitiwa kwa kuwekewa mpango mkakati utakaowezesha kuyatunza maeneo hayo dhidi ya uharibifu wa aina yeyote.

Amesema hayo leo Jumamosi (Disemba 24, 2022) ameongoza kikao cha pamoja na Mawaziri wa Kisekta, Makatibu na Naibu Makatibu wakuu kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa na Wilaya za Morogoro wadau na wasimamizi wa masuala ya ardhi na mifugo ili kutatua, changamoto za usimamizi wa masuala ya ardhi ndani ya Mkoa huo.

Kikao hicho kimefuatia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheahimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Desemba 22, 2022 Wakati akifunga njia ya kuchepusha maji na kuanza ujazaji maji kwenye bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

“Agizo la Mheshimiwa Rais ni lazima litekelezwe kwa sisi wasaidizi kutimiza wajibu wetu na kuweka mikakati ya kutekeleza agizo hilo kwa ufanisi.”

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amewataka wakuu wa Wilaya kuunda kamati za maridhiano baina ya wafugaji na wakulima, ili kutengeneza umoja kati ya makundi hayo mawili “Wafugaji washirikishwe kuandaa miundombinu ambayo wanyama wao wataitumia kupata malisho, maji pamoja na majosho”

Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekemea vitendo vya rushwa kuanzia kwenye ngazi ya viongozi wa Serikali za vijiji “unakuta kiongozi wa kijiji anaruhusu wafugaji kutoka maeneo mbalimbali kwasababu tu amepewa rushwa na anasahau athari ambazo wanazipata wanavijiji wao”

“Jambo lingine muhimu tutambue maeneo yote ya vyanzo vya maji, pamoja na kutambua maeneo ambayo ng’ombe wanaingia katika maeneo ya vyanzo vya maji na kuwaondoa wote ili maji yaendelee kutirika kuelekea katika bwawa la umeme”

Waziri Mkuu amekubaliana na maombi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro la kuwaondoa wafugaji walioko katika eneo la mto kilombero ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Awali, akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa amesema hali ya usimamizi wa ardhi na vyanzo vya maji kwa Mkoa wa Morogoro si ya kuridhisha kwani maeneo mengi ya vyanzo vya maji yameathirika hivyo zinahitajika jitihada za haraka kunusuru hali hiyo.

“Maeneo ya madakio ya maji ya mto kilombero hadi sasa yameathirika kwa asilimia 80 na asilimia 20 iliyobaki ndio inayotegemewa kuzalisha maji katika mto huo tusipochukua hatua sasa hali itakuwa mbaya zaidi.

About the author

mzalendoeditor