Featured Kitaifa

VIONGOZI BEBENI AJENDA YA UKATILI KWENYE VIKAO VYENU-WAZIRI GWAJIMA

Written by mzalendoeditor

Na WMJJWM, DSM

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ametoa wito kwa viongozi hasa wa Kata, Vijiji na Mitaa kuifanya Ajenda ya ukatili wa kijinsia na kwa watoto kuwa ya kudumu katika majukumu yao.

Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito huo alipozungumza na wananchi wa Kata ya Chamazi, Wilaya ya Temeke, Mkoani Dar es salaam ambapo ameshiriki na wananchi hao kuhitimisha madhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na kwa watoto yaliyofanyika kwenye Kata hiyo, Desemba 13, 2022.

Amefafanua kwamba viongozi wana wajibu wa kujadili na kutafuta ufumbuzi kuhusu masuala ya ukatili kama ilivyo kwa masuala mengine ya muhimu kwenye maeneo yao.

Aidha, ameupongeza uongozi wa Kata ya Chamazi chini ya uongozi wa Diwani wa Kata hiyo Mhe. John Gama, kwa kuwa wa kwanza nchini kutekeleza wito wa kuunganisha nguvu za wadau wote pasipo itikadi za kiimani wala kisiasa katika kujipanga kuimarisha mapambano.

“Ndiyo maana Kiongozi namba moja Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema suala la ajenda ya ukatili wa kijinsia, uwezeshaji kiuchumi tulibebe. Hivyo kila kiongozi wa kijamii huko aliko hahitaji kuandikiwa barua ya kutekeleza. Twendeni na Ajenda ya kijamii, twendeni tukayachambue haya mambo tujue tunaishi vipi” amesema Waziri Dkt Gwajima

Ameendelea kusisitiza kuwa bila kujadili Masuala ya kijamii, ukatili haiwezi kuisha. Hivyo amesisitiza mwaka 2023 uwe ni mwaka wa kufanya mapinduzi kwenye vipaumbele vya ajenda za vikao ngazi zote kuanzia mtaa/kata na Halmashauri hadi Taifa.

Waziri Gwajima amesisitiza kuwa, ajenda ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto ikipewa kipaumbele sambamba na kutumika kwa haki ya kisheria ya Halmashauri kutunga sheria ndogo ni Dhahiri mambo mengi yanayochochea ukatili huu wa kijinsia na kwa watoto yanaenda kukoma.

Amehimiza kuwa, pamoja na kuhitimisha siku 16, za Kampeni hiyo inaanza Kampeni endelevu ya siku 365 hivyo, majeshi yote ya jamii ikiwemo SMAUJATA, SKAUTI, GIRLS GUIDE, Majukwaa ya Wanawake, Wajane, wenye Ulemavu, Vijana, Wazazi, Mabaraza ya Wazee na Watoto, Polisi Kata na Dawati la Jinsia, Wasaidizi wa Kisheria, Viongozi wa Dini, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Watoa huduma za Tiba Asili na wengine kwa pamoja chini ya uongozi wa Kamati za MTAKUWWA wakaandae mpango kazi kulingana na mazingira yao kisha taarifa ya utekelezaji iwe inawasilishwa kwenye vikao vyote vya Halmashauri.

Ameongeza pia Halmashauri zione uwezekano wa kutunga sheria ndogo kudhibiti vichocheo vya ukatili huu kwani halmashauri hizo zinayo mamlaka hayo kisheria. Aidha, ametoa wito kila mmoja kuwajibika kwa sababu ufuatiliaji utafanyika ngazi zote.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Chamazi Dafrosa Peter akitoa taarifa ya utekelezaji ya Kata amebainisha kuwa, mwezi Januari hadi Desemba mwaka huu, kata hiyo kwa kushirikiana wadau imepokea mashauri ya ukatili wa watoto 58 yakiwemo ya kingono 12,ya kudhuru mwili 19, utumikishwaji majumbani na maeneo mengine 15 ambapo, mashauri 12 kati ya hayo ymeshughulikiwa, 6 yanaendelea mahakamani na 3 tayari yamepatiwa hukumu.

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia kituo cha Polisi mkoa wa Temeke Meckridige Mwingira amesema
Dawati hilo linafanya kazi na asasi za Serikali na zisizo za Serikali kutoa elimu katika shule za msingi na sekondari katika kata 10 za Wilaya hiyo na kubainisha makosa yanayoripotiwa hasa ni ubakaji, ulawiti, shambulio ya aibu, kutekeleza familia, ukatili wa watoto, ukatili dhidi ya wanaume.

Naye mmoja wa wananchi aliyeshiriki hitimisho hilo amewaasa wazazi kukaa karibu na watoto wao pamoja na changamoto zote za shughuli za kiuchumi wanazokumbana nazo.

About the author

mzalendoeditor