Featured Kitaifa

KITUO CHA KUPOZA UMEME IFAKARA KUKAMILIKA MACHI 2023

Written by mzalendoeditor
 
MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Seif Saidy, akizungumza na waandishi wa habari Ifakara Morogoro (hawapo pichani) kuhusu  utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ifakara na Kilomita 82 za miundombinu ya  usambazaji wa umeme katika Wilaya ya Kilombero na Ulanga.
BAADHI ya Waandishi wa habari Wakimsikiliza Mkurugenzi  Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Seif Saidy,wakati akitoa taarifa ya  utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ifakara na Kilomita 82 za miundombinu ya  usambazaji wa umeme katika Wilaya ya Kilombero na Ulanga.
KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Rodney Thadeus,akiipongeza 
REA kwa kuzidi kuboresha huduma za Nishati kwani huduma nyingi zinategemea umeme. 
MAFUNDI wakiendelea na Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ifakara  ambapo umefikia asilimia 80.1 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2023
MUONEKANO wa Mradi wa  Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ifakara ambapo umefikia asilimia 80.1 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2023
………………………………
Na Alex Sonna-IFAKARA,MOROGORO
MRADI wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ifakara  umefikia asilimia 80.1 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2023 ambapo mpaka sasa tayari transfoma ya kisasa imeshawekwa na kituo kitatoa njia nne za umeme ambazo zitapeleka umeme kwenye maeneo mbalimbali.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Seif Saidy wakati akizungumza na waandishi wa habari Ifakara Morogoro kuhusu kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kituo hicho na Kilomita 82 za miundombinu ya  usambazaji wa umeme katika Wilaya ya Kilombero na Ulanga.
Mhandisi Saidy amesema kuwa mradi umefikia asilimia  80.1 ya ujenzi wake na ulianza kujengwa Machi 2020 na unategemewa kukamilika Machi 2023
”Mradi huu wa kupoza umeme Ifakara utawezesha kupatikana kwa umeme wa kutosha masaa yote, kukomesha kukatika umeme mara kwa mara na kuondoa kero ya kuungua kwa vifaa na mitambo ya umeme.”amesema Mhandisi Saidy
Pia ameema kuwa mradi huo unatarajiwa kuhudumia Wananchi takriban 100,000 wa wilaya za Kilombero na Ulanga.
Aidha ameeleza kuwa wakati REA inaanzishwa mwaka 2007 upatikanaji wa umeme nchini ulikuwa  ni asilimia mbili tu, lakini kwa sasa ni asilimia 69.6  na ifikapo mwaka 2030 umeme utakuwa ukipatikana kwa asilimia 100 yaani vijiji vyote nchi nzima.
“Kwahiyo unaweza kuona mchango mkubwa  wa REA katika upatikanaji wa nishati bora vijijini na jukumu kubwa kupeleka nishati vijijini” amesema Mhandisi Saidy 
Kuhusu kurefusha njia za kusambaza  umeme, Mhandisi Saidy amesema kuwa mradi huo umeshakamilika na njia hizo zenye jumla ya kilomita 82 zitaweza kufikia vijiji na vitongoji takribani 15 katika wilaya ya Kilombero.
Hata hivyo amesema kuwa REA wana Mpango wa kuwezesha uanzishwaji na uendelezaji wa vituo vidogo vidogo vya mafuta vijijini hasa mafuta ya Petroli.
” REA iko kwenye mpango wa kuanzisha programu ya kuwawezesha Wananchi kupata mkopo wa riba nafuu (Riba wezeshi) kwa ajili ya watakaotaka kufanya shughuli ya kufungua vituo vya mafuta vijijini”amesema 
Aidha Mhandisi Saidy amesema kuwa REA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pia wamelenga kusambaza majiko banifu 200, 000 na kuwajengea mitambo ya kuzalisha Bio- Gas katika taasisi za Umma zinazohudumia kuanzia watu 300 hapa nchini ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Mradi huo wa kituo cha kupoza umeme na kilomita 82 za miundombinu ya  usambazaji wa umeme unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Ulaya kwa gharama ya EURO milioni 8.75 ambapo Kituo cha kupoza umeme pekee kimegharimu EURO milioni 5.4.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Hbari-MAELEZO Bw.Rodney Thadeus, amesema mradi wa REA katika ukanda wa Morogoro utasaidia kuhamasisha wakulima kulima.
“Natoa rai kwa Wananchi kushirikiana na Serikali katika kuibadilisha Tanzania kupitia REA ambayo inaendelea kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha wanapata nishati”, amesema Bw. Thadeus.

About the author

mzalendoeditor