Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa usimamizi mzuri wa miradi ya elimu inayotekelezwa mkoani humo.
Kiongozi huyo ametoa pongezi hizo alipotembelea mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya mfano katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma ambapo amesema ujenzi wa Shule hiyo unakwenda kuongeza idadi ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali katika mkoa huo.
“Kwa kweli Dodoma inapendeza ina miradi mingi inatekeleza ikiwemo hii ya elimu, naona inakwenda vizuri. Niseme tu ofisi ya Mkoa tupo tayari kushirikiana nanyi endapo kuna changamoto kuhakikisha miradi hii inakamilika,” amesema Mhe Senyamule.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Serikali imewekeza katika kujenga Shule ya Sekondari mfano kwa lengo la kutoa mfano wa namna miundombinuya shule inapaswa kuwa nchini.
Aliongeza shule hiyo pamoja na kuwa na miundombinu mizuri itakuwa na vifaa vyote, walimu na kwamba pindi ikikamilika itachukua wanafunzi 1,000 wenye vigezo vya kawaida huku ikitoa tahasusi zote.
“Shule hii bado haijapewa jina ila kwa sasa tunaiita shule ya mfano kwa sababu tunataka iwe ni kielelezo cha jinsi shule ya sekondari inatakiwa kuwa kwa miundombinu, vifaa ya kufundishia na kujifunzia, walimu na mahitaji mengine. Hii itasaidia kupima ufaulu wa wanafunzi wanapokuwa kwenye mazingira ya kujifunzia yenye kila kitu,” ameongeza Prof. Nombo.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa ujenzi wa Shule ya Mfano Meja Geofrey Ngole kutoka SUMA JKT ujenzi wa Shule hiyo ulianza Julai 2020 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2022.
Amesema mpaka sasa mradi umetekezwa kwa asilimia 87 na gharama ya mradi ni zaidi ya Sh Bilioni 17.