Featured Kitaifa

WAZIRI KAIRUKI AKERWA NA KASI NDOGO YA UJENZI WA MADARASA TABORA

Written by mzalendoeditor

Na Angela Msimbira, IGUNGA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe.Angellah Kairuki ameonesha kukerwa na kasi ndogo ya ujenzi wa madarasa katika Mkoa wa Tabora.

Kairuki amekutana na kadhia hiyo leo wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku tatu ya kukagua ujenzi wa madarasa yanayojenga kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza 2023 na kubaini Mkoa wa Tabora kuwa nyuma.

Amesema katika ziara yake amebaini kuwa katika halmashauri ya Wilaya ya Uyui ilitakiwa kujenga madarasa 93 na mpaka sasa madarasa 82 yapo nyuma  wakati Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ilitakiwa ujenga madarasa 87 yote yapo nyuma ya kiwango.

Kairuki amesema pia Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua ilipaswa kujenga madarasa 105 lakini madarasa 50 yapo nyuma huku Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ilipaswa kujenga madarasa 29 yote bado yapo nyuma.

Amesema kwa upande wa Halmashauri ya Nzega  walitakiwa kukamilisha madarasa 65 huku madarasa  64 yapo nyuma, Halmashauri ya  Mji Nzega 23 yapo mbele, Halmashauri ya Wilaya ya Igunga 64 yapo nyuma, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora madarasa 68 moja lipo nyuma.

Amesema kuwa Serikali ilitoa ukomo wa madarasa haya kukamilika ifikapo Disemba 15, 2022na Halmashauri nyingi zilianza ujenzi mwezi Oktoba,2022 hivyo kiwango cha ujenzi kilichotarajiwa kwa Mkoa wa Tabora kipo chini.

Kutokana na Hali hiyo, Kairuki ameziagiza Halmashauri za Mkoa wa Tabora kuhakikisha zinaongeza kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuzingatia ubora wa hali ya juu, dhamani halisi ya fedha izingatiwena taratibu nyingine za ujenzizizingatiwe

Amesema ubora wa kazi umezingatiwa ila zipo dosari ndogo kwa kuwa mafundi wanaotumika hawana ujuzi wa kiwango cha juu, hivyo ni wajibu wa wahandisi wa Halmashauri kuwafuatilia kwa karibu kwa kuwasimamia na kuwapa malezi na kutoa mafunzo zaidi na mbinu mbalimbali ili kuweza kuboresha kazi zao.

Kairuki pia mewaomba viongozi wa chama na Serikali kuendelea  kufuatilia kwa karibu ujenzi wa  vyumba vya madarasa 8000 vinavyoendelea kwa sasa  ili watoto watakaochaguliwa kuweza kuingia wote kujiunga na kidato cha kwanza kwa wakati kwa kuwa ni matarajio ya Serikali shule zitaanza katika wiki ya kwanza ya mwezi Januari,2023.

Aidha amewaagiza viongozi wa kata hadi Mkoa kuhakikisha wanasimamia kwa karibu na kutatua changamoto zote zinazojitokeza katika utekelezaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuhakikisha tunafikia adhma ya Serikali.

 

About the author

mzalendoeditor