Featured Kitaifa

ASILIMIA 40 YA WANAWAKE BADO WANGALI KATIKA MADHILA YA UKATILI

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi wa katika soko la Kigogo Freshi, kata ya Pugu, jijini Dar es salaam tarehe 22 Novemba, 2022, kuelekea uzinduzi wa Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia utakaofanyika tarehe 25 Novemba, 2022

Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Jerry Slaa akizungumza na wananchi wa soko la Kigogo Freshi, kata ya Pugu wakati Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipofika kutoa taarifa kwa Umma kuelekea Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia Novemba 22,2022 ambapo uzinduzi utafanyika tarehe Novemba 25, 2022.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigogo Freshi Emmanuel Tarimo akizungumza kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo wakati Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipofika kutoa taarifa kwa Umma kuelekea Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia Novemba 22,2022 ambapo uzinduzi utafanyika tarehe Novemba 25, 2022.

Mkurugenzi wa Shirika la WILDAF Anna Kulaya akitoa salaam za shirika hilo kwa wakazi wa Kigogo Freshi, kata ya Pugu, jijini Dar es Salaam wakati Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipofika kutoa taarifa kwa Umma kuelekea Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia Novemba 22,2022 ambapo uzinduzi utafanyika tarehe Novemba 25, 2022.

Wananchi na wafanyabiashara wa eneo la soko la Kigogo Freshi, kata ya Pugu, jijini Dar es salaam wakifuatilia taarifa kwa Umma iliyotolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kuelekea Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia Novemba 22,2022 ambapo uzinduzi utafanyika tarehe Novemba 25, 2022.

…………………………………..

Na WMJJWM, DSM

Imeelezwa kwamba asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili au kingono mara moja au zaidi katika kipindi cha maisha yao.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, ameyasema hayo akizungumza na waandishi wa Habari pamoja na wananchi katika soko la Kigogo Fresh, Pugu jijini Dar es Salaam tarehe 22 Novemba, 2022 kuelekea siku 16 za kupinga ukatili.

Waziri Dkt. Gwajima amesema taarifa hizo za Utafiti wa Afya ya uzazi na Viashiria vya Malaria inaonesha pia kwa mwaka 2015/16 kwamba asilimia 20 ya wanawake wa umri huo wameingiliwa kimwili bila ridhaa yao.

“Katika kupambana na tatizo la Mauaji na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, jamii yote tunatakiwa kuunganisha nguvu kwenye kubuni mikakati ya kijamii ambayo italeta tija na suluhisho la kudumu. Kwenye maeneo mengi ya nchi kuongezeka kwa uelewa juu ya masuala ya ukatili na madhara yake ni kutokana na utekelezaji wa mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Mwaka 2017/18-2021/22 (MTAKUWWA)” amesema Dkt. Gwajima.

Amebainisha kuwa katika mpango wa MTAKUWWA wa miaka mitano, matokeo chanya yamepatikana kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe na hasa kuwahusisha viongozi wa kijamii wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa kimila, wazee maarufu na watu wengine ambao wana sauti ndani ya jamii.

Ameongeza kwamba, katika kukabiliana na vitendo vya Ukatili wa Kijinsia hapa nchini, Serikali kwa kushirikian na wadau, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili.

Waziri Dkt. Gwajima amewataka wanaume kujitokeza kushiriki kutokomeza vitendo vya ukatili hasa kwa upande wao badala ya kuchukua maamuzi ambayo yana madhara kwa familia na jamii kwa ujumla.

“Serikali kupitia Wizara hii inashughulikia jinsia zote kwa ngazi zote kuanzia Polisi, Magereza, Halmashauri na pia namba 116, elezeni changamoto zenu” ameongeza Waziri Gwajima.

Ameendelea kusema kuwa, kuelekea Siku 16 za Kupinga Ukatili ambapo uzinduzi utafanyika tarehe 25 Novemba, 2022 Serikali kwa pamoja na Wadau itafanya Kampeni katika ngazi zote kuanzia Taifa, Mikoa, Wilaya, Kata na ngazi za Vijiji/Mitaa kulingana na mazingira na taratibu za maeneo husika.

Aidha, amewaasa Wakuu wa Mikoa kutoa Tamko kwa Umma kuhusu uwepo wa Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na Wizara kwa ushirikiano na Wadau wake itafanya ufuatiliaji na kutangaza waliofanya vizuri katika maeneo husika kuhusu mbinu na mikakati ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.

Halikadhalika, Waziri Dkt. Gwajima amesema ngazi zote zinazotekeleza zitaainisha baadhi ya Viongozi wa Serikali, Dini na Kimila, Wataalamu na Watu wenye Ushawishi katika Jamii ambao watakwenda katika vyombo vya habari; luninga na redio hasa redio za kijamii kuzungumzia vitendo vya ukatili wa kijinsia na hasa ukatili dhidi ya watoto katika kipindi chote cha siku 16 za kupinga ukatili.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigogo Freshi Emmanuel Tarimo amesema kwa sasa wananchi wa eneo hilo wengi wana uelewa kuhusu vitendo vya ukatili lakini changamoto ni kutotoa taarifa.

“Serikali inashirikiana vizuri na madawati ya jinsia ya polisi, Pugu, Chanika na Sitakishari, viongozi wa Dini, masuala ya haya yamepungua” amesema Emmanuel

Akitoa salaam za Shirika linaloshughulika na kupambana ukatili wa kijinsia WILDAF Mkurugenzi wa Shirika hilo Anna Kulaya amesema chimbuko la kampeni hiyo ni mauaji ya kinyama ya wanawake wa Mirabelle yaliyofanyika nchini Dominica mwaka 1960.

Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili mwaka huu inaadhimishwa kwa kaulimbiu isemayo “Kila Uhai Una Thamani: Tokomeza Mauaji na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto” na itazinduliwa Mkoani Dar Es Salaam tarehe 25 Novemba, 2022.

About the author

mzalendoeditor