Featured Kitaifa

HISTORIA YAANDIKWA IKUNGI.

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameshiriki mahafali ya kwanza ya darasa la saba ya Shule ya Msingi ya Mbwanjiki na kuwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili watoto wapate elimu bora kama ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),2020/2025, ilivyoahidi.

Shule ya Mbwanjiki awali ilikuwa shikizi kwa miaka 35,ambapo Januari 2022,kwa jitihada za serikali,wananchi na mbunge ilikamilisha majengo na kukidhi vigezo vya kusajiliwa kuwa shule ili kuondoa adha iliyokuwa inawakabili wanafunzi kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita saba.

Akizungumza Novemba 17,2022, katika mahafali hayo Mtaturu aliyekuwa mgeni rasmi amesema kukamilika kwa shule hiyo kumeondoa adha waliyokuwa wanaipata wanafunzi hasa kipindi cha masika.

“Kila mmoja anafahamu historia ya eneo hili,watoto wetu walikuwa wanatembea zaidi ya kilomita saba kwenda shule ya msingi Ikungi,na kipindi cha masika walipata shida kwani kuna mto mkubwa unakatiza kati ya Kijiji cha Ikungi na Mbwanjika,”

“Changamoto hizo zilikuwa zinachangia utoro wa wanafunzi na kuepelekea kushuka kwa taaluma,kama kiongozi nililiona hili na nashukuru serikali imetuunga mkono tumefanikisha ujenzi wa shule hii na matunda yake tunayaona leo,niwapongeze wananchi kwa kupata shule mpya baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 30,”amesema.

Amewashukuru wazee waanzilishi wa wazo Mchungaji Naftal Ngughu na Philipo Ntandu kwa kutoa ardhi ilipojengwa shule hiyo na wananchi kushiriki kwa nguvu zao kuanzisha ujenzi na baadae serikali kuja kutuunga mkono.

“Nawashukuru na kuwapongeza kwa moyo wenu huu,natamani huu moyo wa kushiriki maendeleo mlionao Mbwanjiki usambae jimbo zima,niwaombe wananchi kuitunza shule hii mpya ili iwanufaishe wananchi kwa ujumla,pandeni miti,tunzeni mazingira ya shule ili kuleta madhari nzuri zaidi,”amesema.

“Niwaase wanafunzi wanaoagwa kujitunza wakati mnasubiri matokeo ya mitihani yenu ,wazazi nao mnaowajibu wa kuendelea kuwatunza wanafunzi hawa ili waendelee kupata haki yao ya elimu,”amesisitiza.

Ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea Shilingi Milioni 80 na kuwezesha kujenga madarasa manne na hatimaye kuruhusu shule mpya ya msingi Mbwanjiki kuanzishwa.

“Kama haitoshi tumeletewa Shilingi Milioni 11 za kujenga matundu 10 ya choo,lakini mimi niliwaletea Shilingi Milioni 3 kusaidia kujenga matundu 6 ya vyoo kupitia mfuko wa jimbo,”amesema.

Akizungumzia kuhusu maji Mtaturu amesema tayari kisima kirefu kimechimbwa wanachotafuta ni fedha za kujenga miundombinu ya maji na katika swala la umeme mkandarasi amesambaza nguzo anaelekea kufunga nyaya ili umeme uwashwe.

Mtaturu ametumia hadhara hiyo kuwajulisha wananchi kuwa wamepokea mahindi tani 75 kwenye ghala la Ikungi kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA,ambapo chakula kinauzwa kwa bei nafuu ili kupunguza makali ya bei sokoni na makali ya upungufu wa chakula.

“Niwasihi wananchi kuzitumia vizuri mvua zinazoanza kunyesha ili kujipatia chakula cha kutosha tofauti na msimu uliopita haukuwa mzuri kabisa na kulazimika kuiomba serikali kupitia Waziri wa Kilimo kutuletea chakula cha bei nafuu,”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya shule Joel Isingo amemshukuru sana Mbunge Mtaturu kwa kupambania kuanzishwa kwa shule hiyo tangu akiwa mkuu wa wilaya hadi sasa amekuwa Mbunge.

“Awali alichangia mifuko 50 ya saruji na matofali 750 na baadae Shilingi Milioni 3 za mfuko wa jimbo ili kuunga mkono juhudi za wananchi.,”amesema.

Nae Mchungaji wa Kanisa la KKKT Melkizedeki Mundu amempongeza Mbunge kwa juhudi anazozifanya kuleta maendeleo kwenye kijiji chao,Kata ya Ikungi na Jimbo la Singida Mashariki na kwa ujumla maendeleo yanaonekana kwa macho na sio ndoto.

“Mbunge wetu umekuwa baraka sana toka umeingia ubunge tupelekee salaam kwa Mhe Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio chetu kupitia wewe,”amesema.

Akisoma risala ya wahitimu Nasma Mghenyi ameipongeza serikali kwa jitihada zake na kueleza mafanikio yaliyopelekea kuondokana na changamoto mbalimbali zilizopo shuleni kama upungufu wa matundu ya vyoo, madarasa,walimu,nyumba za walimu, umeme na maji shuleni.

About the author

mzalendoeditor