Featured Kitaifa

WAZIRI BASHUNGWA AMTEMBELEA JENERALI MSTAAFU MWAMUNYANGE

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa (Mb) amemtembelea na kumjulia hali, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange nyumbani kwake Africana Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumjulia hali.
Waziri Bashungwa amemtembelea Jenerali Mstaafu Mwamunyange ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu wake aliojiwekea wa kuwatembelea, kuwajulia hali pamoja na kufanya mazungumzo na wastaafu hao, tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 03 Oktoba, 2022. Mpaka sasa ameshawatembelea Jenerali (Mstaafu) David Bugozi Musuguri na Jenerali (Mstaafu) Raphael Philemon Mboma.
Akiongea wakati wa mazungumzo baina yao, Mheshimiwa Waziri Bashungwa amemweleza Jenerali Mstaafu Mwamunyange kuwa lengo la ziara yake ni kumjulia hali pamoja na kubadilishana uzoefu katika kuiongoza Wizara na Jeshi kwa ujumla, kwa kuwa Jenerali Mstaafu Mwamunyange amelitumikia na kuliongoza Jeshi kwa uadilifu mkubwa.
Aidha, Mheshimiwa Bashungwa ameahidi kuwa ataendelea kushirikiana na viongozi hao wastaafu kwa kuwa ni hazina kubwa kwa Taifa letu pamoja na kuendelea kuwa kiungo imara baina ya Serikali na Jeshi katika kutetea maslahi ya Jeshi na wastaafu hao.
Naye, Jenerali Mstaafu Mwamunyange kwa niaba ya familia yake amempongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu kwa kumteua kuiongoza Wizara hii nyeti, yenye jukumu la kuilinda mipaka ya nchi yetu, katiba ya nchi pamoja na uhuru wa nchi yetu. Kuteuliwa kwake kunatokana na imani kubwa aliyonayo Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu kwake, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Aidha, amemshukuru kwa kutenga muda wake na kuamua kuwatembelea pamoja na watangulizi wake. Kwa kufanya hivyo, kuwapa faraja na kujiona kuwa mchango wao katika Jeshi unatambulika na kuthaminiwa.
Wakuu wa Majeshi waliowahi kuliongoza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu kuanzishwa kwake Septemba 01, 1964 ni pamoja na Jenerali (Mstaafu) Mirisho Sami Hagai Sarakikya (1964 – 1974), Marehemu Jenerali Abdallah Twalipo (1974 – 1980), Jenerali (Mstaafu) David Bugozi Musuguri (1980 – 1988), Marehemu Jenerali Ernest Mwita Kyaro (1988 -1991), Jenerali (Mstaafu) Robert Philemon Mboma (1991 – 2001), Jenerali (Mstaafu) George Mwita Waitara (2001 – 2007), Jenerali (Mstaafu) Davis Adolf Mwamunyange (2007 – 2017) na Jenerali Venance Salvatory Mabeyo (2017 – 2022) na Jenerali Jacob John Mkunda ( 2022 -sasa).

About the author

mzalendoeditor