Featured Kitaifa

 NECTA YATAKIWA KUIMARISHA USIMAMIZI WA MITIHANI NA MIFUMO YA UTOAJI TAARIFA

Written by mzalendoeditor

Bodi mpya ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) imetakiwa kuimarisha usimamizi wa mitihani na mifumo ya utoaji taarifa ili kuondoa changamoto zinazojitokeza katika mitihani.

Akizindua Bodi hiyo Jijini Dodoma leo Novemba 11, 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda ameitaka kusimamia kuimarishwa kwa mfumo wa usimamizi wa uendeshaji mitihani na ule wa upokeaji taarifa za kusaidia Baraza kuendelea kupata taarifa za changamoto mbalimbali ikiwemo za udanganyifu wa mitihani pale inapotokea.

“Kazi kubwa iliyopo ni kuboresha pale walipoachia watangulizi wenu, endeleeni kuboresha mifumo ukiwemo ule wa usahihishaji kielektoniki. Pia tunajua bado kuna changamoto hasa ipo kule tunapopeleka mitihani hivyo Bodi na Baraza endeleeni kufuatilia na kuhakikisha mnasimamia kwa kushirikiana na Kamati husika,” amesema Prof. Mkenda.

Aidha amewataka kupitia Kamati za mitihani kuona kama zinajitosheleza au zinahitaji kuboreshwa ikiwa ni pamoja na kupitia upya vituo vya usahihishaji mitihani.

“Angalieni vituo vya usahihishaji wa mitihani mnavichaguaje na kwa vigezo gani? na kufanya mapitio,” ameongeza Prof. Mkenda.

Prof. Mkenda amempongeza Prof. William Anangisye kwa kuteuliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa Baraza la NECTA pamoja na Wajumbe aliowateua. Aidha amepongeza Baraza lililomaliza muda wake kwa kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa.

Katika hatua nyingine Prof. Mkenda ameendelea kupongeza Baraza la Mitihani la Tanzania kwa kuanzisha mfumo wa E-Marking na kuwataka kuongeza nguvu kwenye kuimarisha usalama na kuhakikisha mfumo huo unapunguza gharama bila kuathiri maslahi ya watumishi, wasahihishaji na wasimamizi.

Mwenyekiti wa Bodi ya NECTA Prof. William Anangisye ameahidi kwa niaba ya Wajumbe wa Bodi hiyo kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri wa Elimu kwa uadilifu na ufanisi mkubwa ili kufikia malengo mapana ya Baraza la Mitihani la Tanzania na Serikali kwa ujumla.

Naye Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma ambae ni Mwakilishi wa Kamati za Mtihani za Wilaya na Mikoa, Upendo Rweyemamu akiongea kwa niaba ya Kamati hizo ameahidi kuendelea kufanya kazi na Bodi mpya na kuwa anaamini Bodi ikiwa
vizuri inawapa nafasi nzuri katika utendaji wao.

Bodi mpya ya Baraza la Mitihani Tanzania imeundwa na Wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na itahudumu kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Julai 2022.

About the author

mzalendoeditor