Featured Kitaifa

SERIKALI: FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO ZITUMIKE KWA MIRADI YA MAENDELEO

Written by mzalendoeditor

Serikali imezitaka halmashauri na mabaraza ya miji Zanzibar kuhakikisha zinatumia fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kwa miradi ya maendeleo kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Hamis wakati akijibu swali la Mbunge wa Nungwi Mhe. Hassan Sadiki Simai bungeni Dodoma leo Novemba 08, 2022.

Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kumaliza malalamiko ya muda mrefu ya ucheleweshwaji wa fedha za Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo upande wa Tanzania Zanzibar.

Mhe. Khamis alisema Mfuko huo upo kisheria namba 6 ya mwaka 2012 ambayo imeelekeza wazi kuwa fedha hizo zpitie katika halmashauri na mabaraza ya miji.

“Mheshimiwa Naibu Spika sheria imeeleza wazi kuwa fedha hizi zitakuwa zinapitia kwenye halmashauri na tulilifanya hili kwasababu ilifika wakati tuligundua fedha nyingi zilikuwa zikitumika kinyume cha utaratibu ndio maana Serikali iliamua sasa zilipitie kwenye halmashauri.

“Lengo la fedha hizi ni kuboresha miradi ya maendeleo katika majimbo husika na si vinginevyo na pia fedha hizo zinapoingia kwenye halmashauri husika wakurugenzi wawajulishe wabunge na pia wahakikishe fedha hizi zintolewa kwa wakati,” alisisitiza Mhe. Khamis.  

Awali akkijibu swali la msingi la  mbunge huyo alisema Serikali imechukua jitihada za kuhakikisha kuwa fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo zinawasilishwa kwenye majimbo ya Zanzibar kwa wakati.

Alisema kuwa mtiririko wa uwasilishwaji wa fedha hizo umekuwa wa kuridhisha, kwa mwaka 2022/23 ambapo sh. bilioni 1,400,000 zimepelekwa Zanzibar Septemba, 2022. 

Aidha, naibu waziri huyo aliongeza kwa kusema kuwa katika mgawango huo wa fedha Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo za mwaka 2021/22 zilipelekwa Zanzibar Oktoba, 2021. 

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chaani Mhe. Juma Usonge Hamad aliyehoji kuhusu kuchelewa kwa fedha za Mfuko huo kwa upande wa Tanzania Zanzibar, Mhe. Khamis alisema changamoto zipo kwenye upande wa Serikali za Mitaa.

Hivyo, kutokana na changamoto hizo aliahidi Serikali itakaa na wakurugenzi wote wa maeneo hayo na kuwaeleza umuhimu wa fedha hizo kwa maendeleo ya wananchi.

About the author

mzalendoeditor