Featured Kitaifa

ASKOFU KINYAIYA:WATOTO NI ZAWADI YA MUNGU NA SI SEHEMU YA NDOA

Written by mzalendoeditor

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap,akimpaka mafuta Matakatifu ya Krisma katika paji la uso  miongoni mwa waimarishwa wa Sakramenti takatifu ya Kipaimara,katika Kigango cha Mt.Augustino wa Hipo-Mtitaa

………………………….

Na Ndahani Lugunya,Dodoma.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya,amefanya ziara ya Kichungaji katika Kigango cha Mt.Augustino wa Hipo-Mtitaa Parokia ya Mt.Maria Immakulata-Bihawana na kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waimarishwa 200 na kubariki ndoa jozi 47.

                                                                          

Katika homilia yake Askofu Mkuu Kinyaiya,amewataka wanandoa na watu wote kutambua kwamba watoto ni zawadi ya Mungu na si sehemu ya ndoa,kwani  zipo baadhi ya ndoa katika jamii zimevunjika kwa sababu ya mwanamke kutozaa watoto.

“Watoto ni zawadi ya Mungu mnaweza mkaoana lakini msipate watoto inawezekana kabisa.kwa hiyo kuzaa kwenye ndoa si sehemu ya Ndoa usiseme hii ndoa haijamilika kwa sababu haina mtoto hapana, mwanaume na mwanamke wakishakutana na kuamua kuishi pamoja inakuwa ni ndoa.Watoto ni zawadi ya Mungu akiamua kuwapa shukuru na asipowapa vilevile shukuru,”amesisitiza Askofu Kinyaiya.

Aidha amewataka wanandoa kujenga utamaduni wa kukaa na kuzungumza mara kwa mara,ili kuondoa tofauti zinazokuepo baina yao.

“Sasa ukiwa na tabia ya kuweka rohoni kila kitu kinapotokea kidogo unahifadhi  husemi hukutani na mwenzako matokeo yake ipo siku kitatokea kingine kidogo sana na hicho kidogo cha mwisho kitafanya ndoa yenu ivunjike kwa sababu ulikuwa na tabia ya kurundika.

Itakuwa kutokuelewana kwa kitu kidogo kunafanya mnaanza kugombana,kutukanana na mwingine kuondoka kumbe mngalikuwa na tabia ya kuzungumza mambo yenu yanapotokea na kuelewana na kusameheana ndoa ingedumu.

Kwa hiyo nawaombeni wanandoa kuweni na tabia hiyo ya kukutana ndugu zangu mwezi usipite hamjakaa wala sio lazima umlazimishe mwanza wako aje mzungumze  bali iwe ni hiari mkae  mzungumze mkifanya hivyo ninaamini kabisa wote ndoa zenu zitadumu  tena na tena,” alisisitiza Askofu Kinyaiya.

Hata hivyo Askofu Kinyaiya amewataka wanandoa kuendeleza yale waliyovutiwa nayo tangu awali kabla ya kuingia katika agano hilo.

Amesema wanandoa yaani mume na mke wanapaswa kutambua kwamba mwenza aliyenaye ni wa kwake,hivyo wanapaswa kuwa pamoja.

Katika hatua nyingine Askofu Kinyaiya amewataka Viongozi wapya waliochaguliwa wa Jumuiya ndogondogo za Kikristo, kuhakikisha  wanajumuiya wanasoma sehemu ya maandiko matakatifu na kutafakari kwa pamoja pindi wawapo jumuiyani.

Amesema umakini na utulivu unatakiwa kuepo kwa kiwango cha juu  pindi maandiko matakatifu yanaposomwa katika Ibada za Jumuiya na hata Kanisani pia,kwani wapo baadhi ya watu huwa wapo hukosa utulivu na umakini wa kusikiliza Neno la Mungu pindi linaposomwa.

“Tunapokwenda kwenye Jumuiya naomba tuanze na Neno la Mungu tusome maandiko na tujiulize hili neno linatubadilishaje sisi katika Jumuiya yetu. kwa hiyo msifike pale mkasali tu Baba yetu na Salamu Maria hapana mnapaswa kutafakari neno na mlisikilize kwa makini.

Na hio iwe mpaka Kanisani kwa sababu nalo hilo ni tatizo wakati masomo yanasomwa kuna watu wanaongeaongea hovyo matokeo yake wanafanya wengine wasifuatilie kwa umakini kwa kuwatazama wao na wao wenyewe hawasikilizi mpaka mwisho,” amesema Askofu Kinyaiya.

Amesisitiza kwamba sehemu ya Maandiko Matakatifu ina umuhimu wa pekee katika Ibada au Misa Takatifu,kama ilivyokuwa katika Liturujia ya Ekaristi Takatifu ambayo ni kilele cha Misa lakini hutanguliwa na Liturujia ya Neno.

“Kwa hiyo naomba tunapokua Kanisani tusikilize masomo kwa utulivu na ninyi wanakwaya wakati wa masomo sio wakati wa kufikiria wimbo gani unafuata mnaanza kelele za madaftari na karatasi za nyimbo, hapana tulia sikiliza masomo ili yatubadilishe ndani kinyume na hapo unaweza ukawa unakuja kila Jumapili Kanisani lakini usibadilike chochote kwa sababu husikilizi masomo wala mahubiri wala sala,” amesema.

Kwa upande wa waimarishwa  wa sakramenti ya Kipaimara Askofu Kinyaiya amesema kwa kuimarishwa kwao kwa Sakramenti ya Kipaimara wamempokea kwa mara ya pili Roho Mtakatifu aliyewashukia mitume siku ya Pentekoste,ili kuwapa uimara, nguvu na ujasiri wa kutoka katika hali ya kujijali wenyewe na maisha yao ya kawaida kwenda kuwasaidia watu wanaowazunguka.

Pamoja na wajibu huo amewataka pia waimarishwa hao kwenda  kuhimiza suala zima la sala za pamoja katika familia ikiwa ni pamoja na sala za asubuhi na jioni,kwani zipo baadhi ya familia za Kikristo hazna utamaduni wa kusali sala za pamoja.

“Muhakikishe kule nyumbani mnasali Sala za asubuhi na jioni wote Baba na Mama na wote wanaoishi pale nyumbani na wewe Mwanakipaimara ndio uongoze sala.na hivyo vitabu vya Katekisumu muendelee kuvisoma ili muelewe vema imani ya Kanisa Katoliki,” amesema.

Askofu Kinyaiya amesema kwamba wapo baadhi ya watu katika jamii kazi yao ni kupinga mafundisho ya Kanisa Katoliki,hivyo waimarishwa wa Sakramenti ya Kipaimara ni askari wa kuilinda na kuitetea imani yao na mafundisho ya Kristo na Kanisa lake.

“Utakutana na watu ambao kazi yao ni kupinga tu mafundisho ya Kanisa kwamba wakatoliki wanaabudu sanamu na wewe utaungana nao kwa sababu hujaelewa mafundisho ya Kanisa.kwa hiyo ni lazime uelewe kwamba hatumuabudu Maria ila tunamheshimu.ukikutana na mtu ambaye haelewi hayo mafundisho mwambie akae kimya na kisha mwelekeze kwa sababu hajui kitu,” amesema Askofu Kinyaiya.

Waimarishwa hao 200 wa mapaji saba ya Roho Mtakatifu na wanandoa jozi 47  ni kutoka katika Vigango vitano vya Kanda ya Kusini mwa Parokia ya Bihawana,ambavyo ni  pamoja na  Kigango cha Isangha,Ibugule,Nyhinila,Chibelela na Kigango cha Mtitaa.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap,akimpaka mafuta Matakatifu ya Krisma katika paji la uso  miongoni mwa waimarishwa wa Sakramenti takatifu ya Kipaimara,katika Kigango cha Mt.Augustino wa Hipo-Mtitaa

Wanandoa takribani jozi 47 kutoka tatika Vigango vitano vya Kanda ya Kusini mwa Parokia ya Bihawana,wakivishana pete za ndoa katika madhehebu ya utolewaji wa sakramenti hiyo (Picha zote na Ndahani Lugunya).

About the author

mzalendoeditor