Featured Kitaifa

MAKATIBU TAWALA WA MIKOA ZISIMAMIENI FEDHA ZA MALARIA

Written by mzalendoeditor

Asila Twaha, OR- TAMISEMI

Serikali imewaelekeze Makatibu Tawala wa Mikoa kuzisimamia fedha za sekta ya afya zikiwemo fedha za malaria zinazopelekwa katika Mikoa yao ili kuisaidia Serikali katika utoaji wa huduma za afya.

Serikali imeeleza hayo Oktoba 20, 2022 katika hafla ya uzinduzi wa miradi miwili ya Dhibiti Malaria na Shinda Malaria itakayotekelezwa kwa Halmashauri 25 katika Mikoa minne kwa lengo la kuendelea kutokemeza malaria nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu (Afya) Bw. Rashid Kitambulilo amesema, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Wadau wa Maendeleo, Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera zinazotungwa na Wizara ya Afya ikiwemo usimamizi katika kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini.

Akifafanua pamoja na jitihada za wadau wa maendeleo kuhakikisha utekelezaji wa afua kinga na tiba za malaria unafanyika na kuleta matokeo chanya katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Bw. Kitambulilo amesema, Serikali itaendelea na jitihada za kudhibiti mianya inayosababishwa na ugonjwa wa malaria kwa kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha ili kutekeleza afua mbalimbali na hasa upuliziaji wa dawa za ukoko katika kuta za nyumba na unyunyuziaji wa viua dudu katika mazalia ya mbu.

Awali Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amesema, bado umakini wa vita dhidi ya mapambano ya malaria unahitajika akielezea takwimu kuonesha bado kuna wagonjwa wanaoenda kupata matibabu kwenye vituo vya afya ambapo wapo wanaogundulika wana ungonjwa wa malaria.

Akieleza kwa mwaka 2021, kuonesha uwepo wa wagonjwa waliobainika kuugua malaria na mwaka 2022 wagonjwa 12 kwa kila wagonjwa 100 wanaolazwa kwenye vituo vya afya wanaugua ugonjwa huo.

“Hii ni changamoto katika nchi yetu tunaipa Serikali mzigo ni lazima tuchukue hatua na nyingine ni kuanza kwa sisi wenyewe kwa kuweka mazingira safi yanayotunzunguka kinga ni bora zaidi”

Kwa upande wa Balozi wa Marekani Dkt. Donald Wright ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kupambana na ugonjwa wa malaria kwa kushirikiana Serikali ya Marekani kupitia PMI kwa kuhakikisha jukumu la kupunguza maambukizi ya malaria kutoka asilimia 18 mwaka 2015 hadi asilimia 7.

Utekelezaji wa miradi hiyo itagharimu dola za Kimarekani milioni 45 ambao itatekelezwa kwa muda wa miaka mitano chini ya Mpango wa Rais wa Marekani wa Malaria (PMI).

Aidha, Miradi ya Dhibiti Malaria na Shinda Malaria itatekelezwa Halmashauri 8 Mkoa wa Ruvuma, Halmashauri 9 Mkoa wa Mtwara, Halmashauri 6 Mkoa wa Lindi na Halmashauri 2 Mkoa wa Pwani.

About the author

mzalendoeditor