Featured Kitaifa

CHUO CHA MIPANGO VIJIJINI CHABAINISHA  VIPAUMBELE VYAKE KATIKA MWAKA WA FEDHA 2022/23

Written by mzalendoeditor

MKUU wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini,Prof.Hozen Mayaya,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 21,2022 jijini Dodoma.

…………………

Na Alex Sonna-DODOMA

KATIKA mwaka wa fedha 2022/23 Chuo cha Mipango ya Maedeleo Vijijini (IRDP) kimetaja  Vipaumbele vyake ambavyo ni pamoja na kuongeza idadi ya udahili na usajili wa wanafunzi kutoka 14,417 mpaka kufikia wanafunzi 16,663 na kuendelea kufanya tafiti na kutoa huduma za ushauri na uelekezi kwa kufanya tafiti saba.

Hayo yamesemwa   leo Oktoba 21,2022 jijini Dodoma Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maedeleo Vijijini (IRDP) Prof Hozen Mayaya wakati akitoa taarifa  kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Prof.Mayaya amesema kuwa chuo hicho kinaendelea kupitia mitaala ya mafunzo ya muda mrefu na kuandaa mitaala ya kozi mpya na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kujenga miundombinu ya kufundishia.

Ametaja vipaumbele vingini ni kuwa a chuo kinaendelea kuajiri watumishi wapya, kulipa stahili mbalimbali, kupandisha vyeo watumishi waliokidhi vigezo pamoja na kuboresha huduma za ustawi na kuongeza uwezo wa kielimu na kiutendaji kwa watumishi 396.

Amefafanunua kuwa chuo hicho kimejipanga kufanya ukarabati mkubwa na mdogo wa nyumba 13 za watumishi, kulipa madeni ya watumishi na watoa huduma, kutekeleza shughuli ambazo hazikutekelezwa katika Mpango Mkakati wa mwaka 2016/17-2020/21 pamoja na uendelezaji wa maeneo ya Miyuji Kaskazini, Chigongwe na Kiseke.

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA CHUO KWA KIPINDI CHA MWAKA WA FEDHA 2021/22

Kuhusu utekelezaji wa majukumu yq chuo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 Prof Mayaya ameeleza kuwa hadi kufikia Juni 2022, jumla ya watumishi 351 walipata mafunzo ya muda mfupi na watumishi 50 wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu ndani na nje ya nchi.

Amesema kuwa Jumla ya Shilingi bilioni 9 zimetumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya uendelezaji na utunzaji wa miundombinu ya chuo ambapo Shilingi bilioni 5 zimetumika katika ujenzi wa kumbi Tatu za mihadhara na mabweni mawili ya wanafunzi wa kike

Ameeleza kuwa kati yai ya Sh.bilioni 9, Shilingi bilioni 4 ambazo ni mapato ya ndani zimetumika kutekeleza miradi katika Kituo cha Mafunzo kilichopo Mwanza ikiwemo ujenzi wa mgahawa, jengo la utawala, maktaba na kununua ardhi kwa ajili ya upanuzi wa chuo.

Sambamba nabhilo ameeleza kuwa Katika mwaka wa masomo 2021/22, chuo kimeendesha program za muda mrefu 31.

“Mpaka kufikia Juni 2022, washiriki 31 wa nje wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi.

“Kwa mwaka 2021/22, chuo kimesajili jumla ya wanafunzi 14,461. Aidha, jumla ya Wahitimu 8,200 wamehitimu mwezi Disemba, 2021

“Katika mwaka wa fedha 2021/22, chuo kiliwezesha wahadhiri wake kufanya tafiti Saba zinazolenga kutatua matatizo ya kijamii, kiuchumi na kuchangia kuandaa sera na miongozo mbalimbali ya kitaifa.

“Chuo kinatekeleza mradi wa “Higher Education for Economic Transformation” ambao umetenga Shilingi bilioni 6.85 kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia, kujifunzia kwa kujenga jengo moja la taaluma, kuboresha mitaala na kuwajengea uwezo Wahadhiri”amesisitiza Prof.Mayaya.

MKUU wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini,Prof.Hozen Mayaya,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 21,2022 jijini Dodoma.

MKUU wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini,Prof.Hozen Mayaya,akisisitiza jambo kwa  waandishi wa habari  kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 21,2022 jijini Dodoma.

About the author

mzalendoeditor