Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI KHAMIS HAMZA KHAMIS AKEMEA UKATAJI MITI OVYO

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amekemea tabia kwa baadhi ya wananchi kukata miti hali inayosababisha uharibifu wa mazingira.

Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lyamidati mkoani Shinyanga wakati Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta wanaoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi ya vijiji 975 walipofika eneo hilo.

 “Tumepita huko tumezunguka tumeona baadhi ya maeneo hayana hata majani lakini tumeviona vishina vya miti kwa maana ya kwamba miti ilikuwepo lakini ilikatwa, sio kwamba wamekuja watu kutoka mbali na kukata hii miti ni siye tuliohamia hapa ndio tumekata miti hii,” alisema. 

Mhe. Khamis aliwataka wananchi waliokata miti katika maeneo hayo na maeneo mengine kuacha mara moja tabia hiyo na kuchukua hatua za kuipanda tena ili kuepukana na ukosefu wa mvua na hivyo kusababisha ukame.

Aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka za Serikali za Mitaa zitahakikisha miche inapatikana ili ipandwe katika maeneo mbalimbali nchini ili kuboresha mazingira. 

Pia aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha maeneo mbalimbali yanapandwa miti na kuitunza ili iweze kukua na hivyo mazingira kuhifadhiwa.

“Ndugu zangu wananchi uhai wetu ni hii miti tunayoina hapa sasa nawaombeni sana ndugu zangu sisi kama Serikali tuko tayari kuwapeni miti ili nanyi pia muipande katika yale maeneo ambayo imekatwa,” alisisitiza. 

Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za kisekta iko katika ziara ya kutembelea mikoa mbalimbali kwa lengo la kutoa mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhususiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

About the author

mzalendoeditor