Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria kuzima Majenereta na kuzindua umeme wa Gridi ya Taifa kwa Mkoa wa Kigoma kwenye hafla iliyofanyika Kasulu Mjini.
……………………………………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Kigoma kuilinda na kuitunza miundombinu ya umeme iliyopita mkoani humo ili iweze kuwaletea manufaa katika shughuli zao za maendeleo.
Rais Samia amesema hayo leo wakati akizindua umeme wa gridi ya taifa na kuzima umeme wa jenereta kutoka megawatt 14 hadi megawatt 20 wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Aidha, Rais Samia amesema kwa hivi sasa mkoa wa Kigoma utapata umeme wa moja kwa moja na wa uhakika ambao utavutia wawekezaji mkoani humo na hivyo kukuza uchumi.
Rais Samia ameendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma ambapo leo amezindua majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga wilayani Kasulu ambayo yamejengwa na Serikali chini ya Mradi wa Kuboresha Mafunzo ya Ualimu Tanzania (TESP).
Rais Samia pia amezindua na kuweka Jiwe la Msingi ujenzi wa barabara ya Manyovu – Kasulu – Kibondo – Kabingo/Kakonko, kufungua barabara ya Kidahwe – Kasulu pamoja na kufungua Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria kuzima Majenereta na kuzindua umeme wa Gridi ya Taifa kwa Mkoa wa Kigoma kwenye hafla iliyofanyika Kasulu Mjini