Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro,akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 12,2022 jijini Dodoma kuhusu sakata la kufeli kwa wanafunzi katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST).
……………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa katiba na sheria, Dk.Damas Ndumbaro ameunda timu ya wabobezi wa sheria saba watakaoongozwa na Dk.Harrison Mwakyembe ambaye amewahi kuwa waziri kwenye Wizara mbalimbali ili kuchunguza tatizo la kufeli kwa wanafunzi wa shule kuu ya sheria.
Waziri Dk Damas Ndumbaro ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata la kufeli kwa wanafunzi katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) ambapo amesema jopo hilo la wataalamu litafanya kazi kwa siku 30 ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo.
Amewataja wajumbe wengine katika kamati hiyo ni Jaji Mstaafu Cililius Matupa aliyewahi kuwa mshauri wa rais Dk Jakaya Kikwete, Rashid Asaa ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma wa Zanzibar.
Wengine ni Gloria Kalabamu, Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Alice Mtulo, Wakili mwandamizi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mary Mniwasa, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dar Stock Exchange na John Kaombwe ambaye ni Mwanafunzi aliyehitimu LST.
”Kuundwa kwa tume hiyo kunakuja baada ya kuibuka kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa Shule Kuu ya Sheria Tanzania (LST) wakilalamika kurudia masomo kwa muda mrefu bila mafanikio.”amesema Dk.Ndumbaro
Waziri amesema kamati hiyo itakabidhiwa hadidu rejea na Kàtibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mary Makondo kesho Oktoba 13, 2022 na itafanya kazi kwa siku 30.
“Baada ya hapo, Mwenyekiti wake atakuja hadharani kutoa taarifa kwa waandishi kuhusu walichobaini lakini muamini kamati ina watu wenye weledi mkubwa sana,” amesema Dk Ndumbaro.
Katika hatua nyingine Dk.Ndumbaro amesema ripoti ya walimu na sifa zao wanaofundisha katika shule hiyo kuu ya sheria ni walimu wazuri na pia ni wabobezi katika masuala ya sheria hapa nchini.
”Punde tu baada ya taarifa hiyo kuibuka,nilimuagiza katibu mkuu kuniletea orodha ya walimu na sifa zao, ambapo nilipokea orodha ya jumla ya walimu 95 ambao kati yao, 14 ni waajiriwa wa kudumu, huku wengine wakiwa ni wahadhiri wabobevu katika masuala ya sheria, wengine wakiwa majaji na mawakili wa serikali. Hii ikiwa na maana kwamba, Shule ina walimu wanaokidhi vigezo.”amesisitiza Dk.Ndumbaro
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro,akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 12,2022 jijini Dodoma kuhusu sakata la kufeli kwa wanafunzi katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST).