Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI MOLLEL ATETA NA MAKAMU WA RAIS TAASISI YA HENRY JACKSON (HJFMRI)  

Written by mzalendoeditor

Na WAF, Dar Es Salaam
 
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel leo amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais na Mkuu wa Oparesheni wa Taasisi ya Henry Jackson (HJFMRI) Bi. Elizabeth Folk (Betsy) inayojishughulisha kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya afya.
 
Akitoa salama kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Mollel ameipongeza Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya afya huku akisema kuwa kupitia ziara ya Kiongozi huyo Serikali inatarajia kuboresha zaidi mahusiano baina ya Tanzania na Taasisi hiyo.
 
Dkt. Mollel amesema Taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Tanzania kufanya tafiti mbalimbali za afya tangu mwaka 2004 kwa kujenga miundombinu ya kutolea huduma za afya, Mapambano dhidi ya UVIKO-19, UKIMWI pamoja na utekelezaji wa afua za matunzo kwa watu wenye VVU.
 
Kwa upande wake Bi. Elizabeth Folk amesema kuwa Tanzania imekuwa mshirika mzuri wa masuala ya tafiti mbalimbali za afya zinazolenga kutoa majibu yatakayosaidia katika upatikanaji wa tiba pamoja na ulinzi wa afya ya binadamu.
 
Amesema HJFMRI imekuwa ikifanya tafiti hizo katika Nyanda za Juu kusini kwa Mikoa ya Mbeya, Katavi, Rukwa, Songwe na Ruvuma huku kwa hivi sasa wakitarajia kutoa msaada wa Dola laki 5 kwa ajili ya mapambano dhidi ya UVIKO-19.
 
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amewasilisha ombi kwa Taasisi hiyo kushirikiana na Serikali kuboresha uwezo wa maabara katika kufanya uchunguzi.
 
Prof. Makubi amesema kuwa Serikali imejenga miundombinu mingi ya kutolea huduma za afya hivyo kuiomba Taasisi hiyo kuwajengea uwezo wataalam wetu pamoja na kusaidia kununua vifaatiba vya maabara.

About the author

mzalendoeditor