Na John Mapepele
Kikosi cha Tembo Warriors leo Oktoba 5, 2022 kimeendelea kuishangaza dunia kwa kuibamiza vibaya timu kali ya Japan katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa Watu wenye ulemavu yanayoendelea nchini Uturuki.
Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini, Mhe Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu wake Dkt. Hassan Abbasi wameongoza kutoa hamasa na mikakati ya ushindi huo wakiungana na watanzania waishio Uturuki.
Katika kipindi chote Tembo Warriors wamekuwa wakicheza kama ndiyo wanaanza mpambano hadi kipenga cha mwisho.
Hadi kipindi cha Kwanza kilipokwisha mabao yalikuwa 1-1 huku Tembo wakiwa wa Kwanza kuliona goli la Japan katika dakika ya 19 ya mchezo.
Japan walilazimisha penati ambayo ndiyo iliyowapatia goli la kufutia machozi.
Akizungumza mara baada ya ushindi huo, Waziri Mchengerwa amesema timu hiyo imeonesha uzalendo mkubwa kwa Taifa lao kilichobaki ni kumalizia kutwaa kombe Kwa kuwa wanauwezo mkubwa wa kurudi na kombe hilo nyumbani.
Aidha, amefafanua kuwa, Serikali ya Tanzania ipo pamoja na timu hiyo katika kila hatua na ndio maana Rais ameridhia kuigharamia timu hiyo kwa kila kitu ili iendelee kufanya vizuri.
“Rais na Serikali yenu ipo pamoja na nyinyi, endeleeni kulipigania Taifa lenu, onesheni uzalendo na kuhakikisha mnarudi na kombe nchini na hiyo itakuwa ni zawadi kwa Rais wenu mpendwa na watanzania wote kwa ujumla ”’ amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Pia, ameendelea kusisitiza kuwa ahadi zawadi nono kwa timu hiyo ikiwemo shilingi milioni 40 endapo watafuzu robo fainali, shilingi milioni 80 wakifuzu kucheza nusu fainali na shilingi milioni 100 wakifanikiwa kufuzu fainali za michuano hiyo ipo palepale.
Amewataka wachezaji kuendelea kuzingatia nidhamu, umoja na kumtanguliza Mungu na kusema kuwa Serikali ipo kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.