Featured Kitaifa

SUA WAREJESHA UOTO KWENYE VYANZO VYA MAJI NA MITO

Written by mzalendoeditor

Mtafiti mkuu wa Mradi huo Prof. Japhet Kashaigili akifurahia jambo wakati alipotembea Kitalu cha Miti Rafiki wa maji kilichoandaliwa na Mradi wake wa EFLOWS katika Kata ya Mdandu Wilayani Wanging’ombe Mkoani Njombe.

………………………..

Zaidi ya Miche 50,000 rafiki wa maji na vyanzo vya mito imeoteshwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira (EFLOWS) kwa lengo la kurejesha uoto wa asili kwenye  vyanzo vya maji vya Mto Mbarali.

Akizungumzia miche hiyo Mtafiti na Mratibu wa Mradi wa EFLOWS kutoka SUA Dkt. Winfred Mbungu amesema kuwa Vitalu hivyo vya miche vimepandwa katika Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya na Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe ambazo Mto Mbarali unaanzia na kuishia.

“Mto Mbarali unaanzia Mkoani Njombe ambako ndiko vyanzo vyake vilipo lakini unapita na kuishia kwenye Wilaya ya Mbarali na maji yake kuingia katika mto Ruaha Mkuu ambapo tumeona kuanzia juu hadi chini kuna unahribifu mkubwa katika vyanzo vyake na kandokando ya Mto kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu hivyo kama mradi tumeona tusifanye utafiti pekee bali tushiriki pia kwenye kurejesha uoto wa asili kwenye eneo lote” alisema Dkt. Mbungu.

Mratibu huyo wa Mradi amesema Mbegu za miche iliyooteshwa imechukuliwa kwenye miti Rafiki ambayo imekutwa kwenye vyanzo hivyo na kandokando yam to ambayo jamii imeipendekeza na kuthibitisha ni miti rafi kwa maji ili kuhakikisha miti yote itakayopandwa iwe miti sahihi isiyoharibu vyanzo na kingo za mito.

Kwa upande wake Mtafiti mkuu wa Mradi huo Prof. Japhet Kashaigili amesema zoezi hilo la upandaji wa miti pia wanashrikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa maana ya kusaidia utaalamu na usimamizi pamoja na Jumuiya za watumia maji Mbarali (JUWAMBA) ili kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja katika kutunza kitalu na miche itakayopandwa ili zoezi liwe endelevu.

“Tunapanda miti hii kama mbegu tuu kwenye mawazo ya watu wote wanaoishi kandokando ya mto huu na vyanzo vyake vya maji waone umuhimu wa utunzaji wa mito kwa maana ya kwamba kama mazingira yatatunzwa vizuri kuanzia mto unapoanzia hadi unapoishia utasababisha kuwe na maji yanayotiririka mwaka mzima lakini pia mto utatiririsha maji ambayo ni salama kwa binadamu wanaoyatumia njiani pamoja na Samaki na wadudu wengine waliomo ndani ya mto na wale walio baharini mto unapoishia” alifafanua Prof. Kashaigili.

Prof. Kashaigili ameongeza kuwa kwa kufanya zoezi hilo kwa vitendo litawasaidia wananchi wote kujua miti inayofaa kupanda kwenye vyanzo vya maji na mito lakini pia kuwajengea uwezo wa kujua faida na umuhimu wa kupanda miti na lakini wanatarajia kupeleka miche ya miti ya matunda ambayo ni fariki wa maji ili waweze kupanda pia kwenye mita 60 za mito ili jamii iweze kujipatia kipato badala ya kupanda miti tuu pekee ambayo haiwasaidii katika uchumi wao.

“Wakati huu ambao tunaeleka mwisho wa mradi maana tumefika nusu ya muda wa utafiti wetu  tunaendelea kufikiria vitu mbalimbali kutokana na Utafiti wetu ili tuache mahali ambapo jamii inaweza kuja kujifunza kwa vitendo masuala ya Uhifadhi wa Mito na vyanzo vyake katika maeneo mbalimbali nchini kuja kujifunza maana changamoto za uharibifu ni kilio kilichopo maeneo mbalimbali ya mito nchini”alieleza Prof. Kashaigili.

Kwa upande wake Mtafiti Msaidizi wa Mradi wa EFLOWS,Bwana  Nyemo Chilagane amesema kuwa kitalu hicho kilianza kuandaliwa mwezi wan ne mwaka huu kwa kushirikiana na JUWAMBA kwa kuokota mbegu za miti aina ya Mizambarau na Mizambarau pori iliyo kandokando yam to na kisha kuiweka kwenye viriba na kuanza kuihudumia hadi sasa ambapo imefikia hatua ya kupandwa.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji (MBUMTILU) Wilayani Wanging’ombe Mkoani Njombe bwana Asheri Kilasi amewashukuru watafiti kutoka SUA kwa kuwezesha kupatikana kwa kitalu hicho kizuri cha miche ya miti Rafiki wa maji kwakuwa wamekuwa wakihangaika katika kutengeneza vitalu bila mafanikio.

Amesema kuwa katika eneo ambalo jumuiya yao inasimamia kuna vyanzo vya mito 176 ambavyo vinachangia maji kwenye mto Mbarali lakini katika vyanzo hivyo vipo ambavyo vina hali mbaya kutokana na kuharibiwa na vipo ambavyo bado vina hali nzuri lakini jitihada zinahitajika katika kuvitunza.

“Kwa sasa tumepata elimu Wanajumuiya wote tunajua mbinu za uoteshaji kitalu na miti inayofaa kupandwa kwenye vyanzo vya maji na kando ya mito na tupo tayari kwa zoezi la kwenda kuipanda maana imeshafikia hatua ya kupandwa ili tuotoshe miti mingine tena lengo letu kubwa ni kuhakikisha Mto wetu na vyanzo vyake vinafunikwa na miti rafiki na maji yanatiririka mwaka mzima maana tunahitaji maji katika shughuli mbalimbali za kila siku kwenye Maisha yetu” alieleza Kilasi.

Kazi hiyo inayofanywa na Mradi wa EFLOWS ni utelezaji wa Programu ya usimamizi endelevu wa Madakio ya maji kupitia tathimini ya kuimarisha mtiririko wa maji kwa mazingira na utekelezaji wake katika kulinda ukanda wa magharibi mwa Bahari ya Hindi kutokana na athari za shughuli za kibinadamu (WIOSAP).

Mtafiti mkuu wa Mradi huo Prof. Japhet Kashaigili akifurahia jambo wakati alipotembea Kitalu cha Miti Rafiki wa maji kilichoandaliwa na Mradi wake wa EFLOWS katika Kata ya Mdandu Wilayani Wanging’ombe Mkoani Njombe.

Mtafiti na Mratibu wa Mradi wa EFLOWS kutoka SUA, Dkt. Winfred Mbungu akifafanua jambo kwa washiriki wa mafunzo ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo wa wa tathimini ya maji kwa mazingira katika nchi za Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi walipokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo.

Hosea Kinyaga (kushoto) akimuonesha Mkuu wa mradi wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili (Kulia) miche aina ya mizambarau inavyoendela vizuri kabla ya kupelekwa kwenye maeneo ya vyanzo ya maji kwa kupandwa.

Washiriki wa mafunzo ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo wa wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira katika Nchi za Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi wakifurahia kufika na kuona Chanzo cha Mto Mbarali katika Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe walipokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo.

About the author

mzalendoeditor