Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA ATANGAZA DIRISHA LA MAOMBI UFADHILI WA ”SAMIA SCHOLARSHIP”

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda,akizungumza wakati akitangaza kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya ufadhili wa Samia Scholarship kwa wanafunzi 640 waliopata ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi katika mitihani ya Kidato cha Sita 2022 leo Septemba 27,2022 jijini Dodoma.

…………………….

Na Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imetangaza kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya ufadhili wa Samia Scholarship kwa wanafunzi 640 waliopata ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi katika mitihani ya Kidato cha Sita 2022 ambapo wanafunzi 43 kutoka Zanzibar watanufaika sawa na asilimia saba.

Tangazo hilo limetolewa leo Septemba 27,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda,ambapo amesema kuwa maombi hayo yataanza  kuwasilishwa kesho kwa njia ya mtandao  kwa siku 14 kupitia tovuti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

Prof.Mkenda amesema kuwa ufadhili huo ni masomo ya shahada ya kwanza kwa wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika mitihani ya Kidato cha Sita mwaka 2022 iliyoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika Tahasusi za Sayansi (PCB, PCM, PGM, CBG, CBA, PMC na CBN).

“SAMIA SCHOLARSHIP itagharamia kwa asilimia mia moja (100%) masomo ya Chuo Kikuu kwa wanafunzi hao ambao wamepata udahili katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba,”amesema.

Waziri Mkenda amefafanua sifa za ufadhili huo kwa wahitimu wa kidato cha sita wenye sifa za uraia halali,ufaulu wa juu kwenye mitihani ya taifa ya kidato cha sita mwaka 2022 iliyoendeshwa na NECTA katika tahasusi za sayansi ikiwa ni pamoja na kupata udahili katika programu za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati au Tiba katika Chuo Kikuu hapa nchini kinachotambuliwa na Serikali.

“Sifa hizi lazima ziwe ambazo zimetajwa katika kundi la kwanza (Cluster 1) katika Mwongozo wa utoaji mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2022/2023 unaopatikana kupitia www.heslb.go,tz ambapo mwanafunzi sharti awe ameomba ufadhili kwa usahihi kwa njia iliyoelekezwa,”.

Hata hivyo Waziri Mkenda ametaja  maeneo ya ufadhili huo kuwa yatazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kugharamia ada ya mafunzo,posho ya chakula na malazi,posho ya Vitabu na viandikwa,mahitaji Maalum ya vitivo na mafunzo kwa vitendo.

Maeneo mengine ni utafiti wa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na bima ya Afya ambapo muda wa ufadhili kwa watakaofadhiliwa, watagharamiwa kati ya miaka mitatu (03) hadi mitano (05) kulingana na programu husika walizodahiliwa.

Waziri Mkenda ametaja masharti ya ufadhili huo kuwa Mwanafunzi atakaepata ufadhili wa SAMIA SCHOLARSHIP atawajibika kuzingatia kusoma, kuelewa na kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Ufadhili wa Masomo kati yake na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuwa na akaunti ya Benki kwa ajili ya fedha atakazolipwa moja kwa moja.

“Mnufaika hataruhusiwa kubadilisha programu ya masomo aliyopatia ufadhili bila barua ya idhini ya maandishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,mnufaika hataruhusiwa kuahirisha masomo, isipokuwa kwa sababu za kiafya, na kuthibitishwa na chuo husika,ikiwa mnufaika ataghairi fursa ya ufadhili kabla ya kuanza masomo, atapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi kwenda kwa Katibu Mkuu,Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Mji wa Serikali Eneo la Mtumba ,”ameeleza

Prof.Mkenda amesema kuwa uchambuzi huo wa wanufaika 640 wa SAMIA SCHOLARSHIP umezingatia uwiano wa Wasichana 244 na asilimia 38% na Wavulana ni 396 sawa na asilimia 62% na kwamba Wanafunzi kutoka shule za serikali ni 396 sawa na asilimia 62% wakati Wanafunzi kutoka shule za binafsi ni 244 sawa na asilimia 38%.

Amesema  kuwa Wanafunzi wenye ufaulu wa juu kiwango cha Alama tatu (3) ni 60 (9%)Wanafunzi kutoka shule za Tanzania Visiwani ni 43 (7%)Wanafunzi kutoka shule za Tanzania Bara 597 (93%)Aidha jumla ya wanafunzi 11 wenye mahitaji maalumu watanufaika na Samia Scholarship.

“Hawa ni asilimia 100 ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu waliopata darala la kwanza katika tahsusi zinazolengwa na Samia Scholarship mwaka 2022/23Shule zilizotia fora kwa kuwa na idadi kubwa za wanufaika wa Samia Scholarship ambazo ni Tabora Boys wanafunzi 79 (12%)St.Mary’s Mazinde Juu wanafunzi 51 (8%)Mzumbe Sekondari wanafunzi 46 (7%)Tabora Girls 39 (6%)Kisimili wanafunzi 31 (5%),”amesema

Kwa upande wake Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Ali Abdugulam Hussein amesema kuwa ufadhili huo utaongeza chachu kwa wanafunzi wengi kusoma masomo ya Sayansi,Teknolojia, uhandisi,Hisabati na Tiba.

“Idadi iliyopo mwaka huu naamini mwakani itaongezeka sana hivyo Mhe.Mkenda kama utaweza kuongea na Mhe.Rais tena aongeze walau Bilion zingine 3 kwa mwakani ziwe 6 kwa sababu naamini idadi itaongezeka maradufu kutokana na hamasa hii,”Amesema Mhe.Ali Abdugulam Hussein

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda,akizungumza wakati akitangaza kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya ufadhili wa Samia Scholarship kwa wanafunzi 640 waliopata ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi katika mitihani ya Kidato cha Sita 2022 leo Septemba 27,2022 jijini Dodoma

SEHEMU ya washiriki wa Mkutano wa Wadau wa Elimu wakimsikiliza Waziri  wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda,wakati akitangaza kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya ufadhili wa Samia Scholarship kwa wanafunzi 640 waliopata ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi katika mitihani ya Kidato cha Sita 2022 leo Septemba 27,2022 jijini Dodoma

Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Ali Abdugulam Hussein,akizungumza wakati wa Mkutano wa wadau wa Elimu mara baada ya kutangazwa kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya ufadhili wa Samia Scholarship kwa wanafunzi 640 waliopata ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi katika mitihani ya Kidato cha Sita 2022 leo Septemba 27,2022 jijini Dodoma

About the author

mzalendoeditor