Featured Kitaifa

SERIKALI KUTANGAZA MAJINA YA WANAFUNZI WALIOPATA UFADHILI KUPITIA ‘SAMIA SCHOLARSHIP’

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ,akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 25,2022 jijini Dodoma akitoa taarifa kuhusu majina ya wanafunzi waliopata ufadhili kupitia ‘Samia Scholarship’.

……………………………..

Na Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda,amesema kuwa Serikali inatarajia kutangaza majina ya wanafunzi waliofaulu vizuri masomo ya sayansi ambao wana sifa ya kupata ufadhili kupitia ‘Samia Scholarship’.

Hayo ameyasema leo Septemba 25,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma.

Prof.Mkenda amesema kuwa Wizara ilitoa ahadi kupitia hotuba ya bajeti ya kuanzisha programu mpya ya kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wahitimu bora wa kidato cha sita katika masomo ya sayansi.

“Septemba 27, 2022 tunafungua rasmi tangazo la wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kufanya mitihani kupitia Baraza la Mitihani Taifa(NECTA) na kufaulu vizuri kwenye masomo ya sayansi ambao wanastahili kupewa Samia Scholarship”

Waziri Mkenda amesema mara baada ya kufungua tangazo hilo majina yao yatatangazwa ambapo mpaka sasa zaidi ya wanafunzi 600  waliofanya vizuri katika masomo hayo wamechaguliwa.

Katika hatua nyingine amesema kuwa Wizara yake imeandaa mkutano wa wadau mbalimbali wa sekta ya elimu kujadili mapitio ya sera na mafunzo ya mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala ya elimu nchini.

Prof.Mkenda amesema kuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe kesho  26 hadi 28 Septemba 2022 Jijini Dodoma.

Waziri Mkenda amesema lengo la Mkutano huo ni kujadili Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mabadiliko ya Mitaa ya Elimu msingi.

”Mkutano huo unajumuisha, Wahadhiri, Waajiri, Wadau wa Maendeleo, Taasisi za umma na Binafsi, Taasisi za Dini, Taasisi zinahusika na uendelezaji wa lugha, Wabunge, Wajumbe toka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Taasisi zisizo za Kiserikali, Jumuiya za kitaaluma, na Taasisi za Sayansi na Utafiti.”amesema Prof.Mkenda

Prof.Mkenda amesema kuwa majadiliano hayo yatatokana na hatua iliyofikiwa katika mapitio ya Sera na mitaala baada ya kukusanya maoni mengi kutoka kwa wadau kupitia mikutano mbalimbali.

About the author

mzalendoeditor