Featured Kitaifa

UPANDISHWAJI HADHI BARABARA KUWA ZA MIKOA UZINGATIE SHERIA – SILINDE

Written by mzalendoeditor

 

Asila Twaha, TAMISEMI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa Mhe. David Silinde (Elimu) ameagiza kufuatwa kwa sheria za barabarani pale barabara zinapofikia kupandishwa hadhi na kuwa barabara za Mikoa.

Ameyasema hayo leo Septemba 20, 2022 Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kusini Mhe. Daimu Mpakate aliyetaka kujua Serikali inampango gani wa kupandisha hadhi barabara ya Tunduru-Masakata hadi Nenjela kuwa ya Mkoa.

Mhe. Silinde amefafanua kuwa, vigezo na taratibu za upandishwaji wa hadhi barabara kuwa za Mikoa au kuteremsha hadhi barabara kutoka daraja moja hadi jingine ni lazima uzingatie Sheria ya barabara namba 13 mwaka 2007 na Kanuni zake ya mwaka 2009.

Aidha, ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kushirikiana na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini(TARURA) kuiangalia barabara hiyo kama imezingatia Sheria,Taratibu na Kanuni za upandishwaji barabara.

Ametoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha maendeleo ya miradi ya barabara, elimu na afya yanaonekana lengo likiwa ni upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Silinde amewaeleza Waheshimiwa Wabunge pamoja na upandishaji hadhi wa barabara za Mikoa unafanyika chini ya Wizara ya Ujenzi Serikali inafanya kazi kwa kushirikiana na itahakikisha barabara hizo zinafanyiwa kazi ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na wananchi.

About the author

mzalendoeditor