Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) wakati wa ufunguzi wa semina ya uelewa wa Kanuni mpya ya mafao ya pensheni iliyofanyika jijini Dodoma.
………………………….
Na: Mwandishi Wetu – Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutatua changamoto za wafanyakazi ili kuboresha maslahi yao.
Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati akifungua semina ya siku moja kwa Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kuhusu uelewa wa Kanuni mpya ya mafao ya pensheni katika ukumbi wa PSSSF, jijini Dodoma.
Amesema kuwa, Rais Samia anawajali na kuwathamini wafanyakazi kutokana na mchango wao mkubwa wanaotoa katika ujenzi wa uchumi wa nchi na ndio maana anataka kila mtumishi aweze kushiriki kikamilifu katika kukuza maendeleo ya nchi.
“Ninyi nyote ni mashahidi katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan watumishi wameweza kupandishwa madaraja vilevile ajira zimetangazwa kwa wingi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu”
“Nimshukuru Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uamuzi wa kulipa shilingi trilioni 2.17 kwa ajili ya kulipa deni lililodumu kwa muda mrefu la shilingi trilioni 4.6 la michango kabla ya 1999 kama malipo ya deni la Serikali kwa lengo la kukomboa mifuko,”
Aidha, Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuwasisitizia viongozi hao wa Vyama vya Wafanyakazi juu ya umuhimu wa kuendelea kutoa na kueneza elimu hiyo ya Kanuni mpya ya mafao ya pensheni iliyoanza kutumika Julai 1, 2022 kwa wanachama nchi nzima.
Sambamba na hayo, Mhe. Ndalichako amewataka viongozi hao kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuleta tija na ufanisi katika kukuza sekta ya kazi na ushughulikiaji wa masuala ya wafanyakazi nchini.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amesema kuwa semina hiyo itasaidia kuwajengea uelewa viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi juu ya Kanuni hiyo mpya ya mafao ya pensheni, ili waweze kukuza uelewa wa wanachama kuhusu kanuni hiyo kwa wanachama wengine.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) wakati wa ufunguzi wa semina ya uelewa wa Kanuni mpya ya mafao ya pensheni iliyofanyika jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakisikiliza maelezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) wakati wa semina hiyo ya uelewa wa Kanuni mpya ya mafao ya pensheni.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Tumaini Nyamhokya akieleza jambo katika semina hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa sekta za Utafiti, Taaluma na Mashirika (RAAWU), Bi. Jane Mihanji akichangia jambo katika semina hiyo.
Mkurugenzi wa Uendeshaji Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Mbaruku Magawa akiwasilisha mada kuhusu Kanuni mpya ya mafao ya pensheni iliyoanza kutumika Julai 1, 2022 wakati wa semina hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akiimba na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wimbo wa Umoja na Mshikamano wakati wa ufunguzi wa semina ya uelewa wa Kanuni mpya ya mafao ya pensheni iliyofanyika jijini Dodoma.