Featured Kitaifa

WAZIRI BASHUNGWA AWAPA KIBARUA KIZITO MA-RC NA MA-DC

Written by mzalendoeditor

OR -TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amewasisitiza Wakuu wa Mikoa kuendelea kushirikiana na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Majiji na Manispaaa kuendelea na zoezi la kutafuta maeneo rafiki ya kujenga miundombinu ya wafanyabiashara wadogo.

Waziri Bashungwa amesema hayo Septemba 14, 2022 katika ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango Jijini Mwanza.

“Wakuu wa Mikoa washirikiane na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi pamoja na Madiwani wa Majiji na Manispaa kuhakikisha wanatafuta maeneo rafiki ya kujenga miundombinu ya vijana na Wamama ambao ni Wafanyabiashara wadogo” amesema Bashungwa

Bashungwa amesema Serikali imetoa maelekezo lengo likiwa ni kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanaboreshewa mazingira kwa kuwapanga katika maeneo maalum ambayo yatawasaidia kufanyabiashara zao.

Aidha, amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima kusimamia Halmashauri ili iweze kutenga fedha za maendeleo na kuboresha maeneo ambayo yameshabainishwa kwa ajili ya kujenga miundombinu ya Wafanyabiashara wadogo katika jiji la Mwanza.

Bashungwa amesisitiza kuwa ni bora Halmashauri itumie gharama kubwa kutafuta maeneo ambayo yatawawezesha wafanyabishara wadogo kufuatwa na Wateja wao, kuliko kujenga miundombinu katika maeneo ambayo sio rafiki kwao.

About the author

mzalendoeditor