Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AZINDUA STENDI YA MABASI MWANZA

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiweka Jiwe la Msingi la Uzinduzi wa Stendi ya Mabasi na Maegesho ya Malori katika eneo la Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza.

………………………………….

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 13 Septemba 2022 amezindua rasmi stendi ya mabasi na maegesho ya malori katika eneo la Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza. Miradi hiyo imegharimu shilingi bilioni 26.6.

Akizungumza mara baada ya kuzindua miradi hiyo, Makamu wa Rais ameutaka uongozi wa mkoa wa Mwanza kutoa vizimba vya biashara vilivyotengwa kwenye Kituo hicho bila upendeleo.

Amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuhakikisha  kunakuwa na uwazi katika utaratibu utakaotumika kutoa vizimba na utaratibu uwe jumuishi ukizingatia makundi maalumu kama wenye ulemavu, vijana na wanawake.

Aidha Makamu wa Rais amewaasa wananchi wote kuhakikisha wanalinda  miundombinu ya Kituo hicho ikiwa ni pamoja na mifumo ya maji, umeme, na vyoo.

Pia ameutaka uongozi wa Manispaa ya Ilemela kuweka huduma madhubuti za kukabiliana na majanga kama moto,huduma ya kwanza pamoja na utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa taka ikiwamo vifaa na teknolojia zinazofaa katika kukusanya na udhibiti wa taka. 

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutoa kipaumbele kwa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji katika Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Ameutaja mkoa wa Mwanza kama mkoa wa kimkakati ambapo amewahakikishia wananchi kwamba viongozi wa serikali wataendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha maendeleo yanapatikana.

Halikadhalika Makamu wa Rais amekemea ujenzi wa vituo vya mafuta kwa kutofuata utaratibu uliowekwa ukiwemo wa mita 500 kila baada ya kituo. Amewataka watoaji wa vibali vya ujenzi kuzingatia sheria na kanuni ili kuepusha maafa yanayoweza kujitokeza kwa wananchi pindi itokeapo dharura ya moto.

Kwa Upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema serikali inatarajia kupeleka bilioni 28.8 katika Manispaa ya Ilemela kwaajili ya kupendezesha jiji la Mwanza kupitia miradi ya Tactic ya Kupendezesha Miji.

Bashungwa amefafanua kuwa mradi huo utajenga soko kuu la kirumba pamoja na barabara zinazozunguka soko hilo zenye kilomita 2.9 ambazo zote kwa pamoja zitagharimu jumla Bilioni 12.7. 

Ameongeza kwamba amesema mradi huo utajenga Barabara ya Buswelu- Busenga – Cocacola yenye urefu wa kilomita 3.3 kwa Kiwango cha lami ambayo itagharimu bilioni 4.6 na barabara ya Buswelu – Nyamadoke – Nyamhongolo yenye kilomita 9.5 itayogharimu bilioni.11.5

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa Miradi hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary amesema miradi hiyo imelenga kuongeza mapato kwa manispaa hiyo, kuvutia uwekezaji pamoja na kuongeza idadi ya wafanyabiashara ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Aidha ameongeza kuwa mradi unatarajiwa kuboresha mazingira ya usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na kuongezeka kwa fursa za ajira ambapo inakadiriwa ajira mbalimbali 1300 zitapatikana.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiweka Jiwe la Msingi la Uzinduzi wa Stendi ya Mabasi na Maegesho ya Malori katika eneo la Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi Stendi ya Mabasi na Maegesho ya Malori katika eneo la Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikagua majengo ya Stendi ya Mabasi na Maegesho ya Malori katika eneo la Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza mara baada ya kuzindua.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizugumza na abiria pamoja na watumiaji wa kila siku wa Stendi ya Mabasi ya Nyamhongolo iliopo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza mara baada ya kuzindua stendi hiyo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia viongozi, pamoja na wananchi mbalimbali mara baada ya kuzindua rasmi Stendi ya Mabasi na Maegesho ya Malori katika eneo la Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza.

About the author

mzalendoeditor