Featured Kitaifa Uncategorized

THTU YAIANGUKIA SERIKALI

Written by mzalendoeditor

Na Alex Sonna-DODOMA

CHAMA  cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) kimeiomba Serikali mambo matatu ikiwemo kuangalia upya tija na ufanisi wa mbinu zinazotumika kukusanya mapato.

Mambo hayo ni tozo  mpya za miamala ya kieletroniki katika simu na benki, sintofahamu ya mfuko wa bima ya afya na ukweli kuhusu nyongeza ya mishahara ya Julai 2022

Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Dk.Paul Loisulie,amesema miezi mitatu imekuwa michungu  kwa wafanyakazi na watanzania kwa ujumla.

“Uchungu huu umetokana na matukio  yaliyojitokeza kwa kipindi hiki ambayo hayakidhi matarajio wala kiu ya wafanyakazi.

“Kwa sababu mambo haya yanagusa maslahi ya wafanyakazi moja kwa moja, yasipoangaliwa yatahafifisha morali ya utendaji kazi na hivyo kuzorotesha utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya Taifa letu.

“Ni ukweli usiopingika kwamba watu na wadau mbalimbali wamejitokeza kusemea, kushauri, kukosoa na pia kutoa njia mbadala ya namna ya kurekebisha au kurudisha hali kuwa ya kawaida. Katika kuendelea kuweka uzito na msisitizo,”amesema Dk.Loisulie

UKWELI KUHUSU NYONGEZA YA MISHAHARA JULAI 2022

Dk.Loisulie amesema Serikali iliongeza mishahara ya kima cha chini kwa asilimia 23.3 mwezi Julai.

“Pamoja na hili kufanyika, upo ukweli ambao ni lazima usemwe ili kutupa nafasi ya kurekebisha wakati ujao.

Amesema tofauti na uzoefu wa miaka ya nyuma, nyongeza ya mshahara kwa mwaka huu ina mkanganyiko mkubwa kwani haijafuata mtiririko na uhalisia uliozoeleka.

Mwenyekiti huyo amesema  baadhi ya wafanyakazi hawajapata nyongeza  hasa wale wenye mishahara binafsi wakati nyongeza ya mishahara huwa inajumuisha watu wote tofauti na nyongeza ya mwaka ambayo ingewatenga wa mshahara binafsi

“Wafanyakazi wote katika mashirika ya umma kama taasisi za elimu ya Juu walipewa nyongeza sawa bila kujali tofauti zao hivyo kupoteza uhalisia wa nyongeza ya kima cha chini.

“Ni ukweli usiopingika kwamba wafanyakazi walio wengi hawajaridhika kabisa na nyongeza iliyotolewa. Kilichopo ni utulivu wa maumivu na sonona na kwamba kumbukumbu hii itabakia.

 “Hali hii inaweza kurekebishwa kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza mishahara kwenye bajeti ya mwaka ujao ambayo maandalizi yake yanaanza hivi karibuni,”amesema.

SINTOFAHAMU YA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA.

Amesema  kabla ya  kumbukumbu ya mishahara isiyoridhisha haijapoa, liliibuka jambo lingine linalohusu sintofahamu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Amesema sintofahamu hiyo  imetokana na kubadilishwa utaratibu wa wagonjwa wanaotumia Bima ya Afya kwenye sharti la uhuru wa kwenda kupima afya au kuwaona madaktari ndani ya mwezi mmoja.

“Bahati nzuri Waziri wa Afya alisitisha utekelezaji wa utaratibu huo lakini haijulikani kitakachofuata baada ya hapo.Tishio la kufilisika kwa NHIF kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni kuzidiwa na mzigo wa gharama za magonjwa yasiyoambukiza pamoja na mambo mengine

 “ Lawama kwa wachangiaji wa NHIF kwamba wanatumia vibaya dhana ya bima ya afya kwa kuwaweka wanufaika wasiohusika kwenye orodha inayotakiwa hasa wenye umri mkubwa ambao wanahitaji matibabu zaidi,”amesema.

TOZO MPYA ZA MIAMALA YA ELEKTRONIKI (SIMU NA BENKI)

Mwenyekiti huyo amesema mwaka jana, serikali kupitia Bunge ilitunga kanuni za kukusanya tozo kutoka kwenye miamala ya simu za mkononi.

Amesema utaratibu huo baada ya kulalamikiwa  serikali ilipunguza viwango na hivyo kuendelea kutozwa.

“Mwaka huu tena kanuni zilitungwa ili kupanua wigo wa kukusanya tozo kutoka miamala yote ya kieletroniki ikiwemo Benki.

“Wadau wengi wameonesha madhara ya tozo katika ustawi wa uchumi na jamii ikiwemo kukata kodi mara mbili kwa wafanyakazi yaani PAYE na tozo yenyewe pia Kukata kodi kwenye kipato ambacho hakijazalisha faida  na Watu wengi kupunguza utaratibu wa kuweka fedha benki ili kukwepa tozo,”amesema.

“Ni wakati muafaka serikali kuangalia upya tija na ufanisi wa mbinu zinazotumika kukusanya mapato. Ernest Hemingway anatukumbusha kwamba “If something is wrong, fix it now”. Tafsiri isiyo rasmi ni kwamba kama jambo haliko sawa litatue sasa.

 “Zaidi sana, ni wakati muafaka Bunge letu kutimiza wajibu wake kwa kuangalia maslahi ya wananchi wanaowawakilisha,”amesema Dk.Loisulie

About the author

mzalendoeditor