Imeelezwa kuwa tabia ya usomaji wa vitabu miongoni mwa watanzania imezidi kupungua na kusababisha uandishi bunifu kudorora.
Hayo yameelezwa Septemba 12, 2022 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Adolf Mkenda (Mb) wakati wa uzinduzi wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ambapo amesema imekuwa janga la dunia hasa baada ya kuwa na mitandao ya kijamii ambayo imefanya watu kupenda taarifa fupifupi.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa hata suala la ukakasi katika uchapishaji na usambazaji wa vitabu nalo limechangia kupunguza ari ya wananchi kupenda kusoma, ambapo amesisitiza kuwa tuzo hizo zitaongeza nafasi ya watu kusoma na kuandika vitabu.
“Hali ya uchapaji, uchapishaji na usambazaji wa vitabu una ukakasi mkubwa ndio maana tumekuja na tuzo hizi ili kufungua ukurasa mpya wa kuchochea tena uandishi, uchapaji, usambazaji na usomaji vitabu hasa kazi za uandishi bunifu” amesema Prof. Mkenda
Kiongozi huyo ameongeza kuwa Serikali imetenga Shilingi bilioni Moja kwa ajili ya kuanza kutekeleza mapendekezo ya wadau ya kutaka Serikali kuchochea uandishi, uchapaji na usomaji vitabu.
Amesema kuwa Tuzo ya Taifa Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu imepewa jina hilo ili kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa Mwandishi wa mashairi na mtafsiri tamthilia.
Prof Mkenda amesema kuwa malengo ya tuzo hizo ni pamoja na kuwatambua kitaifa na kuwazawadia waandishi mahiri, kukuza lugha ya taifa ya kiswahili, kukuza vipaji vya uandishi bunifu na utamaduni wa kujisomea.
Ameongeza malengo mengine ni kuhifadhi historia, amali na mitazamo bora ya Taifa, kukuza Sekta ya uchapishaji wa bunifu nchini na kuongeza hifadhi ya vitabu katika maktaba ya taifa, mikoa, vyuo na shule.
Pia amesema kuwa dirisha la wadau kuanza kutuma kazi litafunguliwa Septemba 13, 2022 na kufungwa Novemba 30, 2022 ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya Shilingi milioni kumi, wa pili milioni saba na watatu atapata kitita cha shilingi milioni tano.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu Prof. Penina Mlama amesema wadau wa uandishi wa vitabu unaona kuwa uamuzi wa Serikali kuanzisha tuzo hizo umeiheshimisha Sekta nzima ya vitabu kuanzia waandishi bunifu, wachapishaji, wasambazji, wauzaji na wasomaji wa vitabu.
Prof. Mlama ametaja nyanja zitakazoshindaniwa kwa kuanzia kuwa ni uandishi wa Riwaya na Mashairi ambapo amewataka washiriki kuchagua eneo moja na kwa riwaya inapaswa kuwa na maneno kati ya 60,000 hadi 100,000 huku kwa mashairi yasipungue kurasa 60 zitakazotumwa tuzonyerere@tie.go.tz