Featured Kitaifa

RAIS SAMIA AWATAKA VIONGOZI KUWAJENGEA UWEZO WANAWAKE NA VIJANA

Written by mzalendoeditor

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia Viongozi mbalimbali wa Ndani na Nje ya Nchi kwenye Kongamano la Wanawake na Vijana wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) lililofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam 

……………………………..

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Viongozi barani Afrika kuendelea kuwekeza zaidi katika rasilimali watu hususan wanawake na vijana. 

Rais Samia ametoa wito huo leo katika Kongamano la wanawake na vijana wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) lililofanyika kwenye ukumbi wa JNICC.

Aidha, Rais Samia amesema uwepo wa nguvu kazi imara utawezesha kutumia vizuri maliasili zetu, kuziongezea thamani, kuendeleza ukuaji wa uchumi na kuwezesha Afrika kuwa na mchango mkubwa katika soko la dunia.

Hali kadhalika, Rais Samia amesema AfCFTA inapaswa kuondoa aina zote za vikwazo vya biashara ili ziweze kufanyika kwa urahisi na kwa kufuata masharti yaliyowekwa na Afrika.  

Rais Samia amewataka Viongozi kutoa msaada wa kutosha kwa wajasiriamali wanawake na vijana ili kushiriki kikamilifu katika biashara na kutumia ipasavyo fursa zitokanazo na soko la Afrika. 

Vile vile, Rais Samia amesema ni muhimu kuwajengea uwezo wanawake na vijana kupitia elimu na matumizi ya sayansi na teknolojia yatakayowawezesha kumiliki na kutumia rasilimali katika kujenga na kukuza uchumi wa Afrika.

Nchi za Afrika zilikubaliana kuanzisha Itifaki ya wanawake na vijana katika biashara ambapo itakapokamilika na kutekelezwa kikamilifu itatimiza lengo la Kifungu cha 3(e) cha Mkataba wa AfCFTA kinachohusu usawa wa kijinsia na kufikia Ajenda ya 2063 ya Afrika Tuitakayo. 

About the author

mzalendoeditor