Featured Kitaifa

TANZANIA, DENMARK KUSHIRIKIANA SEKTA ZA UCHUMI WA BULUU, KILIMO

Written by mzalendoeditor

…………………………………

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimueleza jambo Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Spandet wakati wa mazungumzo yao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Katika jitihada za kukuza na kuendeleza diplomasia ya uchumi, Serikali za Tanzania na Denmark zimeahidi kuendelea kushirikiana katika sekta za uchumi wa Buluu pamoja na Kilimo.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.) alipokutana na Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Spandet katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.  

Waziri Mulamula ameeleza kuwa Ushirikiano wa Tanzania na Denmark ni wa muda mrefu na wa kihistoria hivyo Tanzania itaendeleza  ushirikiano huo kwa maendeleo ya  kichumi na kijamii kwa maslahi ya mataifa yote mawili. 

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mulamula amemuelezea Mhe. Mette Spandet juu ya fursa mbalimbali ambazo ziko Tanzania katika kukuza sekta za uchumi wa buluu na kilimo.

“Tanzania inazo fursa nyingi katika sekta ya Uchumi wa Buluu ikiwemo uvuvi, idadi kubwa ya Samaki na wa aina mbalimbali ambapo ni fursa ya kibiashara, tunazikaribisha kampuni za Denmark kuwekeza kupitia sekta hiyo,” amesema Balozi Mulamula.

Viongozi hao pia wamejadili njia za kuboresha sekta ya kilimo nchini Tanzania ili kuwawezesha Watanzania wengi kunufaika na sekta hiyo hasa ikizingatiwa kuwa asilimia kubwa ya watanzania hutegemea kilimo.

Kwa upande wake Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Spandent ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake na Denmark na kuahidi kuendelea kuudumisha ushirikiano huo katika sekta za kilimo, biashara na uwekezaji, tehama, utalii, demokrasia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.

Katika tukio jingine, Waziri Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya mataifa hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimueleza jambo Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Spandet wakati wa mazungumzo yao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Spandet kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Spandet katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

About the author

mzalendoeditor