Featured Kitaifa

SERIKALI YATANGAZA MSAMAHA KWA ATAKAYESALIMISHA SILAHA HARAMU KWA HIARI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Jumanne Sagini akizungumza wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Kampeni ya Usalimishaji wa Silaha Haramu kwa hiari iliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa, jijini Dodoma,

…………………………..

Na Mwandishi wetu-DODOMA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza msamaha wa kutokushitakiwa kwa mtu yeyote ambaye atasalimisha silaha anayoimiliki isiyohalali kuanzia tarehe 01/09/2022 hadi 31/10/2022 na usalimishaji huo utafanyika katika vituo vya Polisi, ofisi za serikali za mitaa au vijiji kuaniza saa 02:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni na kwamba mtu yeyote atakayepatikana na silaha haramu baada ya muda huo wa msamaha kupita atachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Saginia amesema kuwa suala la ulinzi na usalama ni la muhimu katika maendeleo ya taifa na kwamba silaha haramu zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuvuruga amani ya nchi na kuwataka wananchi wote wanaomiliki silaha kienyeji au kinyume cha sheria wajitokeze kwa wingi kusalimisha silaha wanazomiliki.

“Niwakumbushe kuwa kuendelea kubaki na silaha hizo nimakosa makubwa kwa kuwa zinaweza kutumika kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.Kampeni ya uhamasishaji itasaidia kuwaondoela hofu wananchi na kwamba watakaosalimisha silaha katika kipindi hiki cha msamaha hawatashitakiwa” alisema

Naibu Waziri Sagini aliyasema hayo leo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mwezi wa msamaha wa usalimishaji silaha uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa, jijini Dodoma.

Aidha Naibu Waziri Sagini amewaomba Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini ambao ni wenyeviti wa Kamati za Usalama za maeneo wanayoongoza kusimamia mpango wa uhamasishaji wa wananchi na kuwataka waandishi wa habari kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwahamasisha umma kujitokeza kwa wingi na kusalimisha silaha haramu kwa kipindi cha mwezi Septemba na Oktoba.

“Uhamasishaji ufanyike kupitia viongozi wa dini, mikusanyiko ya kijamii, televisheni na radio, mitandao ya kijamii, vikundi vya ulinzi shirikishi na kubandika matangazo sehemu za mikusanyiko.” Alisema

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura amesema kuwa, hakuna mtu yeyote atakayechukuliwa hatua za kisheria atakaposalimisha silaha kwa hiari katika kipindi kilichotolewa kuanzia tarehe 01 Septemba 2022 hadi 31 Oktoba 2022 na kwamba mtu atakayepatikana na silaha anayoimiliki kwa njia ya haramu baada ya muda huo atachukuliwa hatua za kisheria.

Aidha IGP Wambura amewataka pia wanaomiliki silaha kihalali kuzingatia sheria na kanuni zilizopo ili silaha hizo zisiangukie kwenye mikono ya wahalifu.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Jumanne Sagini akizungumza wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Kampeni ya Usalimishaji wa Silaha Haramu kwa hiari iliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa, jijini Dodoma,

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura akizungumza wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Usalimishaji wa Silaha Haramu kwa Hiari iliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa jijini Dodoma

Naibu Waziri Wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akiteta jambo na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura baada ya uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Usalimishaji wa Silaha Haramu kwa Hiari uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa jijini Dodoma

About the author

mzalendoeditor