Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwenye kikao kazi leo ambapo amewataka wafanye kazi za kutakua kero na shida za wananchi.
…………………………….
Na. OMM Rukwa
Madiwani na Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wametakiwa kushirikiana katika kutatua kero na shida za wananchi ili kuleta ustawi wa mji huo.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga leo (02.09.2022) katika kikao kazi na watumishi kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo mjini Sumbawanga.
“Twendeni tukahudumie wananchi. Tatueni kero zao Kwa wakati . Ni wajibu wenu kuwasiliza ili Manispaa ipate maendeleo” alisisitiza Sendiga
Katika kikao hicho , Sendiga aliagiza Manispaa hiyo iongeze wigo wa ukusanyaji mapato ya ndani ili fedha zipatikane kwa ajili ya utekelezaji miradi ya kijamii ikiwemo shule na zahanati.
Sendiga alibainisha pia anapenda kuona mabadiliko makubwa ndani ya Wilaya ya Sumbawanga na kuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo Sebastian Waryuba kuwasimamia kwa karibu watendaji ili watimize wajibu wao kwa wananchi .
” Mkuu wa Wilaya tumia vyombo vyako vifanye kazi kwa maslahi ya taifa, miradi ya maendeleo ikamilike na fedha za umma zitumike kwa lengo lililokusudiwa na serikali”, alisema Sendiga.
Eneo jingine Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza ni kuhusu sekta ya elimu kuweka mikakati ya kukuza ufaulu na kuepukana na michango inayoleta kero kwa wazazi.
” Nataka kuona ufaulu unaongezeka kwenye Manispaa hii na mkoa kwa ujumla . Walimu wawe wabunifu na mahili kwenye ufundishaji ili wanafunzi wafaulu mitihani yao” alisema Sendiga.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Momoka Mchungaji Charles Chakupewa alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutoa mwelekeo wa namna Manispaa inavyotakiwa kufanya kazi kuleta maendeleo kwa wananchi.
Chakupewa aliongeza kusema wananchi hawapendi kuona miradi isiyokamilika kwenye kata zao.
Kikao hicho ni cha kwanza kwa Mkuu wa Mkoa Queen Sendiga kukutana na kuzungumza na watumishi hao tangu alipoanza kazi Mkoa wa Rukwa mwezi Julai mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwenye kikao kazi leo ambapo amewataka wafanye kazi za kutakua kero na shida za wananchi.