Featured Kitaifa

SERIKALI KUHAKIKISHA MAKUNDI YOTE YANAPATA FURSA SAWA

Written by mzalendoeditor
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju akifungua kikao cha wataalam wa Ustawi wa Jamii wanaopitia Rasimu ya Mwongozo wa uwiano wa kijinsia na ushirikishwaji wa Jamii kinachofanyika jijini Dodoma tarehe 1-3 Septemba, 2022.
…………………………….
Na WMJJWM, Dodoma
Serikali imedhamiria kuhakikisha makundi yote katika jamii yanashiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa Mipango, Sera na Miongozo inayotegenezwa ili kila mmoja anufaike na fursa zilizopo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju alipokuwa akifungua kikao cha wadau wanaopitia na kutoa maoni juu ya kitini cha mwongozo mafunzo ya uwiano wa kijinsia na ushirikishwaji wa Jamii, kinachofanyika Jijini Dodoma kwa siku tatu kuanzia Septemba 01, 2022
Mpanju amesema kitini hicho kitatumika kuhakikisha kwenye huduma zote zinazotolewa nchini zinazingatia uwiano na usawa wa kijinsia na ujumuishaji wa jamii kwa ujumla kwa misingi ya wenye mahitaji maalum.
“Kwa kawaida unapotaka kuongelea Maendeleo na Ustawi lazima uyape mahitaji yake jicho la kipekee ili Maafisa Ustawi na Maafisa Maendeleo ya Jamii wanapotoa huduma kwa jamii wazingatie upekee kwa Makundi hayo  ” amesema Mpanju.
Aidha amemuelekeza Kamishna wa Ustawi wa Jamii kuhakikisha kitini hicho kikikamilika na  kusambazwa kwa wadau wote ili makundi yote maalum yajumuishwe kwenye mnyororo mzima wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii popote walipo kama watanzania wengine.
Akiwapitisha washiriki wa kikao hicho, Mtaalamu Mshauri wa Masuala ya Jinsia kutoka Shirika la PACT Beatrice Sandegea amesema lengo ni kuhakikisha wataalamu wa Ustawi wa Jamii na watoa Huduma ngazi ya Jamii wote kuyatambua matatizo ya kijinsia wakati wa ushirikishwaji wa shughuli mbalimbali za Kijamii na kuyatafutia ufumbuzi.
“Mwongozo huu utaelezea pia namna ya kuingiza uwiano wa Kijinsia ndani ya sera, Mipango na miongozo ya Kitaifa ya huduma za Ustawi wa Jamii na katika Programu za kazi zote, tunapotoa huduma za Ustawi kwa kuzingatia Makundi yote” alisema Beatrice.
Amesema rasimu ya kitini hicho ilifanyiwa majaribio kwa watoa Huduma 110 katika Mikoa 6 na kuonesha ufanisi ambapo waliweza kutambua matatizo na kutafuta namna ya kutatua kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Ameongeza kuwa,  ndani ya jamii ndipo wanapoanza kuwaficha makundi mengine kwa mfano watoto wenye ulemavu hivyo mwongozo unalenga kuhakikisha wanapotoa huduma hakuna mtu anayeachwa.
Kwa upande wake Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Muhando amesema mchakato wa kuandaa kitini hicho ulianza tangu mwezi Juni mwaka huu kutokana na tafiti mbalimbali zilizoonesha kuna changamoto ya ushirikishwaji wa Makundi yenye mahitaji Maalum.
Kikao hicho cha siku tatu kinajumuisha Wadau mbalimbali, Maafisa Ustawi wa Jamii ngazi ya Mikoa sita ambayo Shirika la PACT linafanyia kazi na Maafisa Ustawi wa Jamii wanaotoa Huduma katika ngazi ya Jamii.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju akifungua kikao cha wataalam wa Ustawi wa Jamii wanaopitia Rasimu ya Mwongozo wa uwiano wa kijinsia na ushirikishwaji wa Jamii kinachofanyika jijini Dodoma tarehe 1-3 Septemba, 2022.
Mtaalam Mshauri wa Masuala ya kijinsia kutoka Shirika la PACT  Tanzania Beatrice Sandegea  akiwapitisha wataalamu kwenye  kitini cha mwongozo wa mafunzo kuhusu uwiano wa kijinsia na ushirikishwaji wa Jamii kinachofanyika Jijini Dodoma tarehe 1-3 Septemba, 2022.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera Mhando akieleza lengo la kikao cha wataalamu kupitia kitini cha mwongozo wa mafunzo kuhusu uwiano wa kijinsia na ushirikishwaji wa Jamii kinachofanyika Jijini Dodoma tarehe 1-3 Septemba, 2022.
Baadhi ya wataalam wa Ustawi wa Jamii wakiwa katika kikao cha kupitia rasimu ya mwongozo wa uwiano wa kijinsia na ushirikishwaji wa Jamii kinachofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju katika picha ya pamoja na wataalamu wa Ustawi wa Jamii wanaopitia kitini cha mwongozo wa mafunzo kuhusu uwiano wa kijinsia na ushirikishwaji wa Jamii kinachofanyika Jijini Dodoma tarehe 1-3 Septemba, 2022.

About the author

mzalendoeditor