WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk.Selemani Jafo,
akizungumza na wataalamu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambapo ametangaza kuanza kwa operesheni kabambe ya kutokomeza vifungashio vya plastiki itakayoanza Agosti 29, mwaka huu kwenye Mikoa yote nchini leo Agosti 26,2022 jijini Dodoma.
…………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk.Selemani Jafo ametangaza kuanza kwa operesheni kabambe ya kutokomeza vifungashio vya plastiki itakayoanza Agosti 29, mwaka huu kwenye Mikoa yote nchini.
Hayo ameyasema leo Agosti 26,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na wataalamu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) waliokutana kujadili utekelezaji wa sheria ya mazingira.
Dk.Jafo amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango aliyeagiza mikoa yote nchi kuhakikisha wanapambana na matumizi ya mifuko ya plastiki.
‘Natoa agizo kwa wakuu wa ngazi za mikoa nchini kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) kuanzisha oparesheni maalumu ya kutomeza mifuko yote ya plastiki Agosti 29 mwaka huu”amesema Dk.Jafo
Waziri Jafo amesema lengo la serikali la kuruhusu vifungashio kwa baadhi ya bidhaa ilikua na lengo la kuwasadia wananchi wenye hali za chini lakini hatua hiyo imekua na changamoto kwenye mazingira.
Aidha Waziri Jafo amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe wanashirikiana na viongozi wa masoko na magulio ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama.
“Operesheni hii ikaguse katika masoko,iende ikaguse katika magulio lakini hata hivyo hivi karibuni imejitokeza wazi katika maeneo mbalimbali hasa maeneo ya kuuzia samaki na nyama,vifungashio hivi vimetumika kama kuwa vibebeo,”ameeleza
Hata hivyo Waziri Jafo amewataka wananchi waanze kubadilika kwa kutumia vibebeo sahihi vitakavyokua rafiki kwa mazingira.
Waziri Jafo amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliungana na mataifa mengine kwenye kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa mazingira ikaamua kuja na mkakati wa kuandaa kanuni ya 6 ya mwaka 2019 kwa lengo la kutokomeza mifuko ya plastiki na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk.Samuel Gwamaka, amesema kuwa kamati za ulinzi na usalama kwenye Wilaya na Mikoa zinatakiwa kusaidia suala hilo ili waweze kufanikiwa katika zoezi la oparesheni ya kutokemeza mifuko yote ya plastiki.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk.Selemani Jafo,
akizungumza na wataalamu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambapo ametangaza kuanza kwa operesheni kabambe ya kutokomeza vifungashio vya plastiki itakayoanza Agosti 29, mwaka huu kwenye Mikoa yote nchini leo Agosti 26,2022 jijini Dodoma.
WATAALAMU wa NEMC wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk.Selemani Jafo,wakati akitangaza kuanza kwa operesheni kabambe ya kutokomeza vifungashio vya plastiki itakayoanza Agosti 29, mwaka huu kwenye Mikoa yote nchini leo Agosti 26,2022 jijini Dodoma.