Featured Kitaifa

WAZIRI MHAGAMA ATAKA WATUMISHI TAKUKURU KUZIBA MIANYA YA RUSHWA KWENYE VYANZO VYA MAPATO VYA SERIKALI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa TAKUKURU wakati akifunga mafunzo ya ‘Intermediate Investigation Course’ kwa Wakuu wa Vitengo wa TAKUKURU Makao Makuu, Mikoa na Wilaya yaliyofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani.

…………………………….

Na. Veronica E. Mwafisi-KIBAHA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha wanaziba mianya ya rushwa kwenye vyanzo vya mapato vya Serikali vilivyobuniwa kimkakati ili kuongeza pato la taifa litakalotumika kuleta maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta za kilimo, afya, madini, nishati, utalii na miundombinu.

Mhe. Jenista ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya ‘Intermediate Investigation Course’ kwa Wakuu wa Vitengo wa TAKUKURU Makao Makuu, Mikoa na Wilaya yaliyofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani.

Mhe. Jenista amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kubuni vyanzo vipya vya ukusanyaji mapato ili vitumike kuleta maendeleo nchini, lakini kwenye jambo lolote zuri linapofanywa na Serikali rushwa huwa inajipenyeza hivyo, ni wajibu wa kila mtumishi wa TAKUKURU kujipanga na kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuzuia rushwa isikwamishe mipango ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

“Watumishi wa TAKUKURU tumieni vizuri mafunzo haya mliyoyapata kutekeleza kikamilifu jukumu lenu la kuzuia na kupambana na rushwa kwenye vyanzo vyote vya mapato na miradi ya kimkakati ambayo Serikali imebuni kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Akizungumzia eneo lingine ambalo watumishi wa TAKUKURU wanatakiwa kulipa uzito katika ufuatiliaji, Waziri Jenista amesema ni eneo la fursa za biashara na uwekezaji ambazo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akizitafuta kwa juhudi kubwa ili ziwe na tija na manufaa katika maendeleo ya taifa.

“Mhe. Rais ana mapenzi mema na taifa letu na ndio maana amekuwa mstari wa mbele kutafuta fursa za biashara na uwekezaji ili watanzania wanufaike na fursa hizo kwa kupata huduma bora na kuongeza kipato chao, hivyo hatuna budi kumuunga mkono kwa kutekeleza majukumu yetu kikamilifu katika mapambano dhidi rushwa ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza nchini.” Mhe. Jenista ameongeza.

Waziri Jenista ameongeza kuwa, rushwa isipozuiwa katika sekta ya uwekezaji ni wazi kuwa wawekezaji watakosa imani na kushindwa kuwekeza nchini, hivyo taifa litakosa mapato.

Aidha, Mhe. Jenista ameitaka TAKUKURU kufanya ufuatiliaji na kuchukua hatua stahiki kwa watendaji wasiotenda haki kwa watumishi wanaowangoza, ikiwa ni pamoja na wale wanaoshindwa kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kushughulikia stahiki za watumishi wa umma.

“Tabia za unyanyasaji, upendeleo na mambo mengine yanayokwamisha watumishi wa umma kupewa stahiki zao hazitovumilika, TAKUKURU nawaagiza kufuatilia jambo hili kwa karibu ili watumishi wa umma wasinyimwe haki zao za msingi kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiagiza mara kwa mara ili kuongeza morari ya watumishi kufanya kazi kwa bidIi na uadilifu.” Mhe. Jenista amesisitiza.

Awali, akimkaribisha Waziri Jenista kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha bajeti iliyowezesha watumishi hao kushiriki mafunzo hayo.

“Mafunzo kama haya mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2011 kutokana na ufinyu wa bajeti, lakini Mhe. Rais kwa kuwa aliona kuna umuhimu mkubwa wa watumishi hawa kushiriki mafunzo aliidhinisha bajeti.” CP Hamduni amefafanua.

Mafunzo hayo yamefanyika ili kukidhi matakwa ya muundo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na yamehudhuriwa na Wakuu wa Vitengo wa TAKUKURU wapatao 100 kutoka Makao Makuu, mikoani na wilayani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamisha wa Polisi, Salum Hamduni (wa kwanza kulia) baada ya kuwasili katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani kufunga mafunzo ya ‘Intermediate Investigation Course’ kwa Wakuu wa Vitengo wa TAKUKURU Makao Makuu, Mikoa na Wilaya. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akielekea katika ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani kufunga mafunzo ya ‘Intermediate Investigation Course’ kwa viongozi wa TAKUKURU. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge na kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi Mwalimu Nyerere, Prof. Marcellina Chijoriga.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa TAKUKURU wakati akifunga mafunzo ya ‘Intermediate Investigation Course’ kwa Wakuu wa Vitengo wa TAKUKURU Makao Makuu, Mikoa na Wilaya yaliyofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani.

Sehemu ya Wakuu wa Vitengo wa TAKUKURU wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati akizungumza nao kabla ya Waziri huyo kufunga mafunzo ya ‘Intermediate Investigation Course’ kwa Wakuu wa Vitengo wa TAKUKURU Makao Makuu, Mikoa na Wilaya yaliyofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamisha wa Polisi, Salum Hamduni akiwasilisha taarifa kuhusu mafunzo ya ‘Intermediate Investigation Course’ kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kabla ya Waziri huyo kufunga mafunzo hayo yaliyowashirikisha Wakuu wa Vitengo vya TAKUKURU kutoka Makao Makuu, Mikoa na Wilaya katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi cheti mmoja wa viongozi wa TAKUKURU aliyeshiriki mafunzo ya ‘Intermediate Investigation Course’ yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akipokea tuzo ya kutambua mchango wake katika kuzuia na kupambana na rushwa kutoka kwa mmoja wa washiriki wa mafunzo ya ‘Intermediate Investigation Course’ wakati waziri huyo alipokuwa akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya viongozi wa TAKUKURU walioshiriki mafunzo ya uchunguzi kwa viongozi yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

About the author

mzalendoeditor