Featured Kitaifa

WAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA CANADA BAADA YA KUMALIZA MUDA WA UWAKILISHI

Written by mzalendoeditor
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakifuatilia kikao cha Waziri Mulamula na Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zawadi ya picha Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
…………………..
Na Waandishi wetu, Dar
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), ameagana na Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza na Balozi O’Donnell Waziri Mulamula ameelezea kuridhishwa kwake na utendaji kazi wake ambao umewezesha Serikali ya Tanzania na Canada kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya, elimu pamoja na biashara na uwekezaji.
 
Waziri Mulamula ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Canada ni jambo lililochochewa na kazi nzuri iliyofanywa na Balozi O’Donnell wakati akitekeleza majukumu yake ya kibalozi hapa nchini.
 
“Katika kipindi chako umeiwakilisha vyema Canada na kuonesha mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa na Tanzania na Canada. Kazi yako imechochea uboreshaji wa sekta za afya na elimu pamoja na kuchangia ukuaji wa sekta ya biashara uwekezaji katika nchi zetu, ni matumaini yangu kuwa utaendelea kuwa Balozi mwema kwa Tanzania nchini Canada na kokote uendako Duniani,” amesema Balozi Mulamula.
 
Kwa upande wake Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell amesema anajivunia uwepo wake Tanzania, amejifunza mengi ikiwemo ukarimu wa Watanzania na amewashukuru Watanzania kwa upendo mkubwa waliomuonesha katika kipindi chote cha uwakilishi wake nchini.
 
“Naishukuru Tanzania na watu wake kwa ukarimu na ushirikiano walionionesha wakati natekeleza majukumu yangu ya kibalozi hapa nchini, kwa kweli ni ngumu sana kuaga na kusema kwaheri lakini hakuna budi, siku zote nitakumbuka utu na ukarimu wa Watanzania,” amesema Mhe. Balozi O’Donnell.
 
Pamoja na mambo mengine, Balozi O’Donnell ameihakikishia Tanzania kuwa Canada itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta ya gesi pamoja na biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili.
 
“Wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Canada wamekuwa wakiridhishwa na mazingira ya biashara na uwekezaji na baadhi yao wameonesha nia ya dhati ya kuwekeza katika sekta ya gesi Tanzania,” ameongeza Balozi O’Donnell
 
Kadhalika, Balozi O’Donell amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Tanzania ya kuimarisha ukuaji wa Uchumi, utoaji wa huduma bora za afya, elimu ya msingi bure kwa watanzania pamoja na kuboresha miundimbinu kwa maendeleo ya watanzania.

About the author

mzalendoeditor