Featured Kitaifa

MZEE BAHARI SEIF ALIYEVAMIA ENEO LA MAKAZI YA WAZEE NUNGE KIGAMBONI ATAKIWA KUBOMOA MARA MOJA NYUMBA ZAKE MBILI

Written by mzalendoeditor

Na WMJJWM, Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju amemuamuru Mzee Bahari Seif ambaye amevamia eneo la makazi ya Wazee Nunge yaliyopo Kigamboni Mkoani Dar Es Salaam kubomoa mara moja nyumba zake mbili alizojenga katikati ya eneo hilo bila kibali cha Serikali.

Amri hiyo imetolewa leo tarehe 09/08/2022 baada ya kikao kati ya Wizara na uongozi wa Wilaya hiyo kilichokuwa na lengo la kujadili utatuzi wa changamoto za makazi hayo.

Mpanju akizungumza wakati akitoa agizo hilo amewataka wafawidhi wa Makazi ya Wazee yanayosimamiwa na Wizara nchini kufanya kazi kwa ushirikiano na mamlaka zilizopo ili kutatua mapema changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

“Makazi haya yapo chini ya Wizara lakini usimamizi wa kila siku ni Mamlaka zilizopo kwa maana ya Ofisi ya Rais TAMISEMI hivyo shirikianeni na viongozi hawa” alisema Mpanju

Aidha, Mpanju amewaelekeza wapangaji wa nyumba hizo kuhama na kuwataka wananchi wanaofanya biashara eneo la makazi kuacha mara moja kwani eneo hilo sio la biashara bali ni Makazi ya kuwatunza Wazee wasiojiweza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Fatma Nyangasa amesema wataendelea kusimamia kwa pamoja makazi hayo na kuhakikisha changamoto zinatatuliwa na atalisimamia zoezi la kuhama wapangaji wa nyumba zilizoamriwa kubomolewa.

“Tutafuata taratibu zote kuhakikisha Mzee huyu anaondoka eneo la makazi na kusimamia makazi haya kwani yapo kwenye eneo letu” alisema Mhe. Fatma.

Kwa upande wake Mzee Bahari Seif amekubali na kutii amri hiyo na ameahidi kuondoka katika eneo hilo kwa kubomoa nyumba zake mbili ambazo ameweka wapangaji kwa sasa.

About the author

mzalendoeditor